Maonyesho ya Ngoma za asili yatakayofanyika katika Mikoa ya Zanzibar Kaskazini (Nungwi), Kusini (Jambiani), na Mjini Magharibi (Kisonge)
Busara Promotions ni Taasisi inayoandaa tamasha la muziki la Sauti za Busara mara moja kwa mwaka ndani ya Mji Mkongwe, tunapenda kutangaza mipango mipya ya maonyesho yatakayofanyika kisiwani hapa mwezi wa Tisa na Kumi: Maonyesho haya yanajulikana kwa jina la “Sauti Zetu”
Tamasha hili dogo limeandaliwa ili kusherekea na kutangaza utamaduni wa Zanzibar na kuwapatia nafasi wasanii na wanamuziki wazawa. Vikundi vitakavyoshiriki katika maonyesho haya vitapata nafasi ya kushiriki katika tamasha la Sauti za Busara februari 2014, Rebecca Corey Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotions alisema kuwa watapata nafasi ya kujulikana kitaifa na kimataifa na kujenga mahusiano kwa utamaduni wa ndani wa Zanzibar.
Journey Ramadhan, Mmoja wa waandaji wa Busara Promotions, alisema”maonyesho haya ya kikanda ni muhimu kwa Busara ili kuongeza uelewa wa kazi zetu katika mikoa mingine ya Zanzibar ( Nje ya Mji Mkongwe) na kujenga mahusiano mazuri na watu na wasanii wa kisiwa hiki. Pia ni muhimu kwa wasanii kwa sababu itasaidia kukuza vipaji vyao, kuwafanya wawe wajasili na kuwaongezea miundombinu. Pia ni nafasi muhimu kwa watazamaji wa nje ya Mji Mkongwe kuona ambavyo Sauti za Busara inavyowatangaza wasanii wazawa, katika maonyesho haya yote pamoja na tamasha la Sauti za Busara. ’Sauti Zetu’ itawaonyesha watazamaji kuwa vikundi vitakavyo shiriki katika maonyesho haya ya Mikoa yao ni wasanii bora.”
Maonyesho haya ya kikanda “Sauti Zetu” yatafanyika wiki hii Jumamosi tarehe 21 Septemba 2013 Nungwi na yatashirikisha vikundi vya ngoma za asili kama vile: Kidumbaki, Dumu, Mchikicho, na Pungwa. Maonyesho haya yataanza saa tisa mpaka kumi na mbili katika shule ya msingi ya Nungwi. Kiingilio ni BURE kabisa.
Maonyesho haya yameandaliwa kwa ushirikiano na Maafisa Utamaduni wa Wilaya za Kasikazini A, Kasikazini B na Afisi ya shehia ya Nungwi.
Kati ya mwezi wa tisa na wa kumi Busara Promotions itaandaa maonyesho mengine katika Mikoa ya Mjini Magharibi (Kisonge) na Kusini (Jambiani). Tarehe husika itatangazwa hapo baadae.
Busara Promotions ipo katika maandalizi ya toleo ya 11 la tamasha la muziki la Sauti za Busar, litakalo fanyika kuanzia tarehe 13 mpaka 16 February 2014, ndani ya Mji Mkongwe, Zanzibar.
Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Mkurugenzi mtendaji wa Busara Promotions, Rebecca Corey, kupitia barua pepe hii: rebecca@busara.or.tz.
Shukran za dhati kwa : Royal Norwegian Embassy, Hivos, Goethe Institute, Memories of Zanzibar, Azam Marine, Ultimate Security, Zanzibar Unique Ltd., SMOLE II pamoja na wadhamini na wahisani wetu wote wa Sauti za Busara 2014.