Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Serikali yaombwa kutafuta njia ya kuyauza Majenereta ya dharura

$
0
0
 Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO} Thabit Salum Khamis akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  mfumo mpya wa huduma za umeme unaotumika katika kituo kikuu cha Umeme kilichopo Mtoni wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya huduma za umeme Nchini.
 Mhandisi  wa Vituo vya Umeme katika shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Mohd Juma Othman akimfafanulia  Balozi Seif mfumo wa ugawaji wa laini za umeme mkubwa kwenda katika vituo vipya vilivyojengwa kwa lengo la kutoa huduma za uhakika za Umeme maeneo tofauti Nchini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea maendeleo ya uzalishaji wa umeme kupitia miundo mbinu iliyopo hivi sasa kwenye kituo kikuu cha umeme Mtoni.
Kulia ya Balozi ni Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban na kushoto yake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Zeco Thabit Salum Khamis.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji Nishati na Madini imeombwa kufikiria njia muwafaka ya kuyauza Majenereta yaliyopo katika kituo kikuu cha kupokelea Umeme Mtoni ili kuwepusha hasara endapo yataendelea kuwepo eneo hilo bila ya matumizi.
 
Majanareta hayo 30 yalikuwa yakitoa huduma za umeme wa dharura katika kipindi ambacho Zanzibar ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa huduma ya nishati ya umeme kutokana na kianzio chake ilichokuwa ikikitumia wakati huo kutokidhi mahitaji halisi ya huduma hiyo Nchini.
 
Mhandisi wa Maganareta katika Kituo Kikuu cha Umeme Mtoni Yussuf Reja alitoa ushauri huo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuangalia maendeleo ya uzalishaji wa huduma ya umeme Nchini kupitia miundo mbinu iliyopo katika kituo hicho.
 
Mhandisi Yussuf Reja alimueleza Balozi Seif kwamba Majenereta hayo yako katika kiwango  bora lakini tatizo kubwa liliopo ni huduma ya mafuta ambayo ni maalum { IDO } na yana  hitaji  gharama kubwa za uendeshaji.
 
Alisema Shirika la Umeme lilikuwa likipata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni 16,000,000/-  kwa saa wakati majenereta hayo yalipokuwa yakiwashwa kusaidia huduma za umeme katika kipindi cha mgao wa huduma hiyo muhimu.
Mhandisi Yussuf Reja alifahamisha kwamba shirika la umeme lilikuwa likizalisha umeme kupitia Majenereta hayo kwa  uniti moja yenye  thamani ya shilingi 500/-  ambayo ingelazimika kuwauzia wateja wake uniti moja kwa shilingi 700/- gharama ambayo ni mzigo kwa mwananchi wa kawaida.
“ Ukweli uliowazi gharama ya kuyaendesha Majenereta hayo kupitia shirika la Umeme ni kubwa mno na inaweza kuleta maafa kwa shirika hilo endapo yataendelea kutumiwa “. Alitahadharisha Mhandisi Yussuf Reja.
 
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Nd.Mustafa Aboud Jumbe alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wizara hiyo tayari imeshapokea mapendekezo ya Shirika hilo kuhusiana na majenereta hayo ya Kituo cha Umeme Mtoni.
 
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Ardhi  Mustafa Jumbe alisema Wizara hiyo inajipanga kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na baadaye kuyawasilisha Serikali kuu kwa ajili ya kupatia ufumbuzi muwafaka.
 
Mapema Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Thabit Salum Khamis alisema mfumo mpya wa kisasa wa huduma za umeme kwenye kituo kikuu cha Umeme Mtoni uitwao { SCADA } umewawezesha watendaji wa shirika hilo kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
 
Thabit Salum alimfahamisha Balozi Seif kwamba mfumo huo umepunguza kero kubwa ya kukatika katika kwa umeme kulikokuwa kukitoa usumbufu kwa wananchi walio wengi kwenye maeneo mbali mbali wakati inapotokea hitilafu.
 
Alieleza kwamba shirika la umeme limekuwa na vituo vikubwa vinavyosambaza umeme kutoka kituo kikuu cha Mtoni kwenda Welezo na Fumba ambavyo vimepangwa kusambaza huduma hiyo na kuacha mfumo wa zamani wa kutumia laini moja tu.
 
Kaimu Meneja huyo wa Shirika la Umeme aliongeza kwamba matumizi zaidi ya  umeme huongezeka kutoka Mega walts 33.16 nyakati za asubuhi hadi kufikia  Mega Walts 48.1 kipindi cha  jioni lakini huduma hiyo kuongezeka zaidi katika kipindi cha siku kuu na kufikia hadi Mega Walts 52.
 
Uwezo wa laini mpya ya umeme uliopo Zanzibar hivi sasa imefikia Mega Walts mia moja  ambapo shirika limekuwa na hakiba ya umeme kwa zaidi ya asilimia 50% mbali ya ile laini ya zamani yenye uwezo wa mega walts 40 kutokana na kuchakaa kwake.
 
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwatanabahisha watendaji wa shirika la umeme kwamba huduma ya umeme hivi sasa imekuwa nyenzo  muhimu ya kiuchumi kwa vile inasaidia kipato cha mwananchi.
 
Balozi Seif alisema ni vyema kwa watendaji wa shirika la umeme kufanya kazi zao katika mazingira ya ushindani mfano wa kuwepo  mashirika mengine yanayotoa huduma hizo hapa nchini kwa lengo la kupata ufanisi sambamba na kutoa huduma bora kwa wateja wake.
 
“ Watendaji lazima mfanye kazi kama mko katika ushindani wa kibiashara  na mashirika mengine licha ya kwamba mpo peke yenu. Kila mkiamka lazima mfikirie mtaongeza vipi wateja wengine wapya “. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya athari na hatari ya kutumia mafundi wa mitaani katika kuungiwa huduma hiyo jambo ambalo mara nyingi huleta hasara kutokana na hitilafu zinazojitokeza baadaye


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>