STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21 Novemba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wazee, watendaji na viongozi wa CCM wa ngazi mblimbali kukutana mara kwa mara na viongozi wa Serikali kuzungumzia na kuelimishana juu ya mafanikio na changamoto zinazoikabili jamii badala ya kusubiri kuziwasilisha changamoto hizo kwa viongozi wa kitaifa pekee.
Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wazee wa mkoa wa Kaskazini Pemba katika mkutano uliofanyika huko Wilaya ya Micheweni katika mkoa huo.
Alisema inapendeza zaidi kuona kuwa mambo yanayoweza kuzungumzwa na kutolewa ufafanuzi au kupatiwa ufumbuzi na viongozi katika ngazi za wilaya yanawasilishwa kwao kwa lengo la kuyatambua na ikibidi kuyapatia ufumbuzi badala ya kusubiri kupelekwa kwa viongozi wakuu wa Chama na Serikali
Aliwakumbusha wazee na viongozi kuwa Katiba ya CCM na Jumuiya zake zimeweka misingi mizuri na imara katika kuendesha chama na kwamba endapo itafuatwa ipasavyo masuala mengi yanaweza kupatiwa ufumbuzi katika vikao husika.
Dk. Shein alihimiza ushirikiano kati ya viongozi, watendaji na wanachama wa CCM katika kutekeleza malengo ya chama hicho na kutahadharisha juu ya baadhi ya watu ndani ya chama kutaka kuhodhi mamlaka ya chama hicho.
Alisema ni lazima wana CCM wabadilike kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na kuimarisha mshikamano wao kwa kuwakumbusha kaulimbiu ya chama hicho ya “Umoja wetu ndio ushindi wetu”.
Halikadhalika aliwakumbusha wazee wajibu wao wa kulea vijana wa chama hicho ili wawe watiifu na wepesi wa kukitumikia chama chao.
Katika mkutano huo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alirejea tena wito wake kwa wananchi kuisoma na kuielewa vyema Katiba ya chama chao na katiba ya nchi mbayo ndiyo msingi wa Sheria za nchi.
Aliwahakikishia wazee hao kuwa Serikali haiwezi kumuacha mtu mmoja au kikundi cha watu kuvunja sheria na kuvuruga amani na utulivu na kusisitiza kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
Aliongeza kuwa hivi sasa Serikali inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ndiyo iliyotumika kuombea kura na kusisitiza kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kuleta maendeleo nchini hivi sasa ni utekelezaji wa Ilani hiyo.
Dk. Shein aliwaeleza wazee hao kuwa ni kweli kuwa Ilani ya uchaguzi ilielekeza kuimarishwa kwa hospitali ya Micheweni kuwa ya Wilaya na kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa kwa kuipatia hospitali hiyo maabara ya kisasa pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi wake.
Awali wazee hao katika risala yao walimpongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM hadi sasa.
Risala hiyo ilieleza kuwa katika mkoa wa Kaskazini Pemba utekelezaji wa ahadi unaendelea vizuri na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Saba kwa kutimiza miaka mitatu tangu ilipoingia madarakani.
Wazee hao vilevile walimpongeza Rais kwa ujasiri wake mkubwa wa kusimamia amani na utulivu nchini.