Rais mstaafu Dkt. Salmin Amour aliwahi kutoa changamoto kwa mafundi wa kuchonga wa vikozi vya SMZ kwa kuwataka waende Ikulu ndogo ya Kibweni kuangalia fanicha zilizokuwemo ili wazichonge tena. Fanicha za kibweni ni za kizamani sana zenye ufundi wa hali ya juu. Mafundi wa JKU waliibuka kuiga fanicha moja tu nayo ni meza ndogo, fanicha zilizobakia ziliwashinda kuzichonga. Meza hii hadi leo mafundi wa JKU wakiichonga wanauza kwa bei ya juu. Aina hii ya changamoto ndiyo inayosaidia kuleta maendeleo ya nchi. Wataalamu wetu wengi hatuwatumii ipasavyo lakini leo sisi wananchi wa Meli Nne tunataka kuwatumia.
Sisi wa Meli nne tunatoa changamoto kwa wafanyabiashara akiwemo ndugu yetu bwana Bahresa, wahandisi wetu na wananchi wote wa Zanzibar kuligeuza eneo hili linalotuwama maji hapo Mwanakwerekwe kwa kutumia elimu ya uhandisi na fedha kuligeuza eneo hili na kuwa viiwanja vya kupumzikia kwa sisi watu wa Meli nne na vitongoji vyake. Sisi tunaamini eneo hili litasaidia sana vijana wetu kujiajiri kama litageuzwa kuwa bustani pamoja na kuwa na sehemu za kuuzia bidhaa za vyakula kama chips, urojo n.k. Kwa kifupi tunaowaomba wahandisi na wawekezaji wa ndani wakutana kutafuta njia eneo hili kuwa "FORODHANI YA MELI NNE" Ziwa hili la Mwanakwerekwe ni karaha tupu. Uchafu unaotupwa hapa hauleti haiba ya mji wetu wote wa Zanzibar. Kwa kuwa sehemu hii ipo njia; imezagaa uchafu; na hakuna anayejali, inatuwakilisha vibaya kuwa"sisi watu wa Zanzibar ni wachafu wa daraja la kwanza"
Ikulu ya Marekani huna maofisa wanaoshughulikia zawadi tu "gift officers" Wakati umefika mji wetu kuwa na "makungwi" wanaoshughulikia namna ya kuupamba mji wetu ili uvutie. Mji wetu ni mzuri lakini kama mwali aliyekosa kungwi haupendezi na miongoni mwa mambo yanayochusha ni ziwa hili la Mwanakwerekwe. Hebu angalieni picha hizi zaidi:
Maelezo na picha na Mohammed Muombwa mkaazi wa meli nne