Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein aagiza utoro maskulini ukomeshwe

$
0
0

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                              22 Novemba, 2013
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemuagiza Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba kwa kushirikiana na Kamati ya Maendeleo ya Skuli ya Msingi ya Kengeja kukomesha kabisa tatizo la utoro linaloikabili Skuli hiyo.

Agizo hilo amelitoa jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Kengeja katika Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba mara baada ya kuzinduzi madarasa mapya saba ya Skuli hiyo.

“Uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na Kamati ya Maendeleo ya skuli, ufuatilie kwa karibu suala la utoro na kuweka kumbukumbu za kila hatua zinazochukuliwa kwa kuonyesha idadi ya watoto waliorejeshwa skuli” Dk. Shein alieleza.

Kwa upande mwingine Rais aliwataka wazazi kufuatilia kwa karibu mahudhurio ya watoto wao na kwamba wasiridhike kuona watoto wao wanaondoka nyumbani na kuanga wanakwenda skuli.

“wazazi wasiridhike kuwaona watoto wao wanaondoka nyumbani kwenda skuli lakini hawana budi kufuatilia maskulini kuona kama wanahudhuria masomo, kujua maendeleo yao na kufahamu wana matatizo gani” Dk. Shein alifafanua.

Katika maelezo yake ya awali kwa Mheshimwa Rais, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Awali Bi. Zahra Ali Hamad alieleza moja ya changamoto inayoikabili skuli hiyo ni utoro ambao unamfanya awe anaitembelea skuli hiyo karibu mara tatu kwa mwaka.

Sambamba na agizo hilo Mheshimiwa Rais alikemea tabia ya baadhi ya wazazi kuwaoza watoto wa kike bado wakiwa wanafunzi kitendo ambacho alikieleza kuwa ni cha kuwanyima watoto hao fursa ya kujiendeleza kimaisha.

“Msiwape waume watoto wakiwa bado skuli. Mnawanyima fursa yao ya kujiendeleza. Wapeni fursa wajiandae na maisha yakiwemo hayo ya majukumu ya kifamilia”Mheshimiwa alisisitiza.

Aliwaeleza wazazi na walezi kuwa Serikali inatoa fursa maalum kwa watoto wa kike kujiendeleza kimasomo na hivi karibuni imerejesha skuli maalum kwa ajili yao tu dhamira ikiwa ni kupata wanawake wataalamu wa fani mbalimbali.

“Tumetoa upendeleo maalum kwa watoto wa kike kwa kuwapatia skuli mbili maalum lengo letu likiwa ni kuandaa mabingwa wa taaluma mbalimbali” Dk. Shein alieleza na kuwataka wazazi wawaache watoto wazitumie fursa hizo kikamilifu.

Aliwakumbusha wananchi umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya mtu binafsi na kwa Taifa na kueleza malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo moja ya lengo lake lilikuwa kuondoa ubaguzi katika elimu ili kuhakikisha kila mwananchi anapata elimu.

Aliwapongeza wananchi wa Kengeja kwa ushirikiano wao katika ujenzi wa madarasa wa skuli hiyo na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake katika kuimairsha miundombinu ya elimu.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Bi Zahra Ali Hamad alisema kuwa wazazi na wanafunzi wana haki ya kujivunia kukamilika kwa madarasa hayo kutokana na kuimarika kwa mazingira ya kusomea.

Alifafanua kuwa skuli hiyo ilipoanzishwa kufuatia kugawanywa kwa skuli ya Kengeja kuwa skuli mbili ya Sekondari na Msingi, ilikosa vifaa muhimu ikiwemo madawati.

Akitoa maelezo katika hafla hiyo Afisa Mdhamini wa Wizara ya Elimu Maalim Mohmaed Iddi alieleza kuwa skuli hiyo imejengwa na wananchi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wahisani wakiwemo Shirika la Misaada ya Sweden-SIDA.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>