Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein : Wahudumieni wananchi bila ya ubaguzi

$
0
0

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                              24 Novemba, 2013
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Viongozi na watendaji wa Serikali kisiwani Pemba wamekumbushwa kuwa ni wajibu wao kutoa huduma bora na bila ya ubaguzi kwa wananchi, wakijua kuwa wao ni watumishi wa umma wanaowajibika kwa wananchi wote.

Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana alipokuwa akizungumza na  viongozi na watendaji wa Serikali wa ngazi ya wilaya , mkoa na Maafisa Wadhamini wa Wizara ikiwa ni hitimisho la ziara yake ya siku sita kisiwani Pemba.

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu ndogo Chake Chake, Rais aliwakumbusha viongozi na watendaji hao kuwa cheo ni dhamana ambayo inawawajibisha kuwatumikia wananchi hivyo wanatakiwa kuwa makini katika utendaji ili kuleta ufanisi katika utoaji huduma.

Dk. Shein pia alisisitiza haja ya kuongeza umakini katika usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma ikiwemo fedha za Serikali ili kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa hoja za kiukaguzi ikiwemo kuundiwa Tume za mara kwa mara kuzichunguza wizara na Idara za Serikali.

“Maafisa Wadhamini, Wakuu wa Mkoa, na Wilaya pamoja na makatibu tawala wa wilaya na mikoa lazima msimamie rasilimali za Taifa. Tunataka Serikali ipate hati safi za matumizi yake ”alieleza Dk. Shein.


Aliwataka viongozi na watendaji hao wa Serikali kuimarisha ushirikiano ambao ni muhimu katika kipindi hiki ambacho Serikali imo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

“Ni mfumo mpya kwetu na mgumu wa uendeshaji wa Serikali lakini hadi sasa tumejitahidi pande zote mbili na tumefanikiwa hivyo nanyi imarisheni ushirikiano miongoni mwenu ili muweze kutoa huduma kwa wananchi” Dk. Shein aliwaambia.

Aliwakumbusha viongozi na watendaji hao kuwa wanapaswa kuzingatia suala la uwazi katika utendaji wa Serikali kwa kuelimisha wananchi juu ya mipango ya Serikali, mafanikio ya utekelezaji na changamoto zake ili kuwawezesha wananchi kushiriki vyema katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini.

“Uwazi katika utendaji hivi sasa ni jambo linalopewa nafasi kubwa katika uendeshaji wa Serikali ulimwenguni hivyo Serikali yetu haina budi kuwaeleza wananchi kila kinachofanyika kwa manufaa yao na Taifa” Rais alieleza.

Aliongeza kuwa kabla ya kwenda kwa wananchi viongozi na watendaji hao wanapaswa kuwa wawazi miongoni mwao na huku akisisitiza kuwa ni lazima kiongozi na mtendaji ayafahamu kwa kina masuala anayoyasimamia katika wizara au taasisi yake na kuwa tayari wakati wote kujibu hoja au kufafanua jambo linalohusu Wizara au Idara yake.

“Tuwaeleze wananchi mipango yetu, utekelezaji wake na changamoto zake na viongozi muwe na taarifa za kutosha kuhusu shughuli mnazozisimamia ili unapohitajika uweze kutoa maelezo stahiki” Dk. Shein alisema.

Kuhusu rushwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwataka viongozi na watendaji hao wajiepushe na suala la rushwa pamoja na ubadhirifu wa mali za Serikali.

Alisema Serikali tayari imeanzisha mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar na haitapendeza kwa viongozi au watendaji wa Serikali kuhusishwa na vitendo vya rushwa.

Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali iko makini sana katika kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayowasilishwa serikalini.

Akizungumza na wazee wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika hoteli ya Hifadhi iliyopo katika mji wa Chakechake Dk. Shein amewahakikishia wazee hao kuwa malalamiko ya wananchi yanafanyiwa kazi na Serikali kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Serikali inasimamia haki ya kila mwananchi na ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo”alieleza Dk. Shein.

Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwahakikishia wazee hao kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa iko imara na ndio maana  Zanzibar imeshuhudia mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Saba.  

Rais amemaliza ziara yake ya siku sita kisiwani Pemba jana na anatarajiwa kurejea Unguaj leo. Katika ziara hiyo alifuatana na Mke wake mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Haji Omar Kheri, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Haruon Ali Suleiman, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk na Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Issa Gavu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles