Na Mwajuma Juma
TIMU ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ imeagwa jana na kukabidhiwa bendra ya Zanzibar na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis kwa ajili ya kwenda nchini Kenya katika mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayoanza Novemba 27 mwaka huu.
Kikosi hicho cha wachezaji 20 kitakuwa chini ya Mkuu wa Msafara Faida Salmini na kocha wao Salum Bausi kinatarajiwa kuondoka kesho asubuhi kwa ndege ya Kenya 540 Fly.
Hafla ya kuagwa kwa timu hiyo ilifanyika huko katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani na kutakiwa kuweka mbele nidhamu wakati wote wakiwa katika michuano hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo Bihindu alisema kuwa nidhamu ni kitu muhimu na ambacho kinaleta ambapo ndio itakayoleta ushindi kwa timu yao.
Hivyo aliwataka kujenga matumaini mema na viongozi walioambatana nao kwa kuwasikiliza kila wanalowaelekeza.
“Muondoke hapa mukiwa na nia moja ya kwenda kuleta ushindi kwani mukileta ushindi itakuwa ni miongoni mwa shamra shamra za kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar”, alisema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa bendera Nahodha wa timu hiyo Khamis Mcha Viali amesema kuwa wanakwenda huko kwa kazi moja tu ambayo ni kuleta ushindi.
Alisema kuwa watajitahidi wanaweka mbele nidhamu na kuwaomba Wazanzibari wazidi kuwaombea duwa ili waweze kufanikisha malengo yao.
“Tunaondoka hapa na nia moja ambayo ni ya kwenda kushindana na sio kushiriki”, alisema.
Zanzibar Heroes inaondoka ikiwa na msafara wa watu 26 wakiwemo wachezaji 20 na viongozi sita inatarajiwa kutupa karata yake ya kwanza Novemba 27 kwa kucheza na timu ya Sudani ya Kusini wakati wa saa 8:00 mchana katika uwanja wa Nyayo.