Mkurugenzi wa Wizara ya Afya Zanzibar ambae pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Malik Abdalla Juma amelazwa katika Hospitali ya Agakhan ilioko Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Tukio la kujeruhiwa Mkurugenzi huyo limetokea jijini Nairobi wakati alipokuwa akihudhuria Mkutano wa Elimu endelevu ya Udaktari.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Saleh Jidawi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi ofisini kwake Mnazi mmoja mjini Unguja.
Alisema Daktari huyo amejuruhiwa katika sehemu ya kichwa na macho na kumsababishia kupata maumivu mwilini mwake.
Aidha alisema mara tu ya kutokea kwa tukio hilo Daktari huyo alikuwa amelazwa katika hospitali ya Kenyatta kwa matibabu ya awali lakini hivi sasa amehamishiwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
Hata hivyo alisema Serekali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya itahakikisha kwamba Dkt.Malik anaangaliwa chini ya maandalizi ya madaktari mabingwa wa upasuaji wa ubongo (Neuro Surgeons) ili waweze kujua athari zilizojitokeza baada ya kupata mara majaraha na kupatiwa huduma zinazofaa kwa wakati muwafaka.
Sambamba na hayo alisema kwamba serekali itagharamia gharama zote za matibabu yake zinazostahiki huku na kupeleka ujumbe wa watu wane ambao utaongozwa na Katibu Mkuu na Mkurugenzi na watu wawili kutoka katika familia yake.
Katibu Jidawi amesema hivi sasa ni mapema kueleza jambo lolote katika hatua ya zinazoendelea katika kupatiwa matibabu, hivyo baada ya kufika huko na kurejea kwao ndio watatoac taarifa zaidi.
Mbali na hayo baadhi ya watu waliosafiri nchini Kenya ambao hawakupenda kutaja majina yao walisema wao wakati walipokuwa Nairobi nchini Kenya walipewa tahadhari na madereva wa texi, kuwa hivi sasa kumekuwa na matukio ya kihalifu.
Walisema miongoni mwa tahadhari waliopewa za kutembea nyakati za jioni katika baadhi ya mitaa, pia asiwe mtu mmoja pekee yake katika matembezi yake.