STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 27 Novemba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuimarisha masuala ya utafiti kwa kuwa majukumu ya msingi ya Wizara hiyo yanategemea zaidi tafiti.
Kwa hiyo amesema Wizara haina budi kuzingatia, katika kupanga bajeti yake, umuhimu na uzito wa shughuli za utafiti ili kuleta uwiano wa vipaumbele katika mipango ya wizara.
Aliitaka Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuchangamkia masuala ya utafiti hata kama ni kwa kuwashajiisha watafiti kutoka nje ya Wizara hiyo.
Dk. Shein ambaye alisema hayo wakati akihitimisha Kikao cha Kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara hiyo kwa mwaka 2012/2013 aliikumbusha Wizara hiyo kuendeleza ushirikiano wa karibu na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kulitafutia ufumbuzi tatizo la bei ndogo ya zao la mwani.
Alibainisha kuwa imekuwa jambo jema wananchi wameitikia wito wa Serikali wa kuendeleza kilimo cha mwani na kuifanya Zanzibar sasa kuwa nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa mwani hivyo ni lazima jitihada zifanywe kulitafutia ufumbuzi tatizo la bei kabla ya wananchi hawajakata tamaa.
Akitoa maelezo ya awali ya Wizara yake katika kikao hicho Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdillah Jihad Hassan alieleza kuwa Wizara yake kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 iliweza kutekeleza malengo yake kwa ufanisi wa asilimia 64.
Waziri alifafanua kuwa idara ya Mipango, Sera na Utafiti ilitekeleza malengo yake kwa asilimia 72, Idara ya Uendeshaji na Utumishi asilimia 81, Idara ya Huduma za Utabibu wa Mifugo asilimia 59, Idara ya Uzalishaji Mifugo asilimia 77, Idara ya Maendeleo ya Uvuvi asilimia 47 na Idara ya Mazao ya Bahari asilimia 85.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho Wizara imetoa huduma mbalimbali kwa walengwa ili kuimarisha maendeleo ya Mifugo na Uvuvi nchini.
Alibinisha kuwa wastani wa wafugaji 34,000, wavuvi 38,000, wazalishaji wa mwani 21,000 na vikundi 146 vya wafugaji wa mazao ya baharini wamefaidika na huduma hizo.
Waziri alikieleza kikao hicho kuwa Sekta ya mifugo ilikuwa kwa asilimia 3.1 na kuchangia asilimia 4.2 ya pato la Taifa mwaka 2012 huku sekta ya uvuvi ilikuwa kwa asilimia 2.3 na kuongeza mchango wake kwa pato la Taifa kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011 hadi asilimia 7.1 mwaka 2012.
Aliongeza kuwa sekta ya Uvuvi imezidi kuimarika kutokana na kuongezeka kwa uvuvi wa baharini na ufugaji wa samaki na mazao ya baharini.
Alieleza kuwa jumla ya tani 9.7 za samaki waliovuliwa kutoka mabwawa ya wananchi mwaka 2012 tani 7.7 zilivuliwa Pemba ikilinganishwa na tani 2.0 katika kisiwa cha Unguja.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad mbali ya kuipongeza Wizara hiyo kwa mafanikio iliyoyapata kwa mwaka uliopita lakini aliitaka Wizara hiyo kuchukua jitihada za makusudi za kuhimiza ufugaji wa kuku ili kuondoa kadhia ya kuagiza kuku kutoka nje.
“Wizara lazima ifanye jitihada maalum kuhimiza ufugaji wa kuku wote wa kienyeji na wa kisasa hivyo uongozi wa Wizara hauna budi kuweka malengo ya kuongeza ufugaji wa kuku hatua kwa hatua ili kukidhi mahitaji ya nchi”alisisitiza Maalim Seif.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Kassim Gharib alikifahamisha kikao hicho kuwa Wizara katika kipindi kilichopita imekamilisha kazi ya kufanya tafsiri ya Sera ya Mifugo katika lugha ya Kiswahili na kuchapisha nakala 1000 ya sera hiyo 500 zikiwa kwa lugha ya kiswahili na nyingine 500 kwa lugha ya kingereza.
Katika kuimairisha miundombinu ya mifugo alieleza kuwa watendaji 5 wa Wizara walitembelea maabara kuu ya mifugo iliyoko Temeke Mkoa wa Dar es Salaam na vituo vya utafiti wa mifugo Tanga, Arusha na Dodoma.
Wizara pia alieleza kuwa ilianza mchakato wa ujenzi wa Machinjio ya Kisakasaka kwa kumuajiri Mchoraji na Msimamizi wa machinjio hayo.
Kuhusu utafiti wa maradhi ya mifugo Wizara alisema iliweza kufanya tafiti mbalimbali zikiwemo za maradhi ya kutupa mimba kwa ng’ombe ambapo sampuli za damu 58 za ng’ombe wa maziwa zilikusanywa kwa uchunguzi na pia kufanya uchunguzi wa maradhi ya kiwele cha ng’ombe.
Kwa upande wa chanjo Wizara iliweza kutoa chanjo ya maradhi ya vibuma/matukwi kwa ndama 113 na kuchanja kuku 38,925 dhidi ya ugonjwa wa mahepe.
Akizungumzia juu ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya baharini Dk. Kassim alibainisha kuwa Wizara katika kipindi hicho huko Pemba ilivitembelea na kuvipa ushauri wa kitaalamu jumla ya vikundi 88 vya ufugaji wa mazao ya baharini, wakulima wa mwani katika vijiji 33 na kampuni 7 za mwani.