STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 27 Novemba , 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto imetakiwa, katika siku zijazo, kuingiza katika Mpangokazi wake utafiti wa masuala ya unyanyasaji wa wanaume, hali ya watoto ombaomba pamoja na hali ya watu wenye ulemavu.
Agizo hilo limetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana wakati akihitimisha mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara hiyo kwa mwaka 2012/2013 na robo mwaka ya mwaka wa fedha 2013/12014.
Alisema Serikali imelivalia njuga suala la mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia nchini na kuitaka Wizara hiyo kuyafanyia kazi ipasavyo matokeo ya utafiti iliyoufanya kuhusu suala hilo.
Aliipongeza Wizara hiyo kwa kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimeweza kuonyesha changamoto katika maendeleo ya jamii nchini hususan unyanyasaji wa kijinsia lakini akaitaka Wizara kupanua wigo wa utafiti huo kwa kujumuisha suala la unyanyasaji wa wanaume unaofanywa na wanawake katika jamii.
Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa Wizara kuimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmini ili Wizara iweze kufanya vizuri zaidi huku akihimiza kuwatumia watumishi wenye uwezo na ujuzi katika eneo hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alieleza kuwa ametiwa moyo na mpango wa Wizara wa kufanya utambuzi wa watoto walio katika mazingira magumu hivyo akaitaka kuandaa mpango madhubuti ambao utavutia pia taasisi nyingine kusaidia watoto hao.
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad alitoa wito kwa Wizara hiyo kuendelea kufanya shughuli zake kwa umakini zaidi kwa kuwa inashughulikia wananchi walio katika makundi maalum yanayohitaji uangalizi na huduma maalum.
Wakati huo huo Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto katika mwaka fedha 2013/2014 inakusudia kutekeleza malengo makuu saba.
Akizungumza kabla ya kuwasilisha taarifa ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Bi Zainab Omar aliyataja miongoni mwa malengo hayo kuwa ni pamoja na kuongeza na kutanua programu za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, kuyafanyia kazi mapungufu katika Sheria na Sera zinazohusu watoto, Wanawake, Vijana na Wazee na kukuza uwezo wa Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Sambamba na malengo hayo Waziri alieleza kuwa vipaumbele vikuu vya wizara kwa mwaka 2013/2014 ni pamoja na kujenga utamaduni wa ujasiriamali na kuimarisha uwezo wa wajasiriamali hususan vijana na kuandaa mazingira mazuri ya kisera na kisheria ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha uratibu wa Hifadhi ya Jamii, kutoa mikopo kwa vikundi vya kiuchumi na watu binafsi na kusimamia urejeshaji wa mikopo pamoja na kuratibu uzingatiaji wa masuala ya jinsia katika mipango, bajeti na programu na pia kusimamia mapambano dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia.
Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Wizara kwa mwaka wa fedha uliopita Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi Asha Ali Abdalla alieleza kuwa Wizara yake ilikamilisha tafiti tatu ambazo ni za masuala ya udhalilishaji kijinsia, sababu za kuongezeka kwa kiwango cha talaka Zanzibar na sababu zinazopelekea ombomba.
Katika utafiti wa unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto matokeo yameonyesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa kote Unguja na Pemba ambapo udhalilishaji wa kingono unaongoza kwa asilimia 80 huku ikionyesha kuwa wafanyaji wa vitendo hivyo ni walimu wa skuli na madrasa, ndugu wa karibu wakiwemo baba, kaka,wajomba na asilimia kidogo wageni.
Utafiti huo kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu imezidi kubainisha kuwa vitendo hivyo hufanyika zaidi majumbani kwa asilimia 46.7, njiani asilimia 37.6 na skuli na madrasa asilimia 14.5.
Kwa upande wa sababu za kuongezeka talaka utafiti umegundua kuwa tatizo hilo lipo kwa asilimia 31.8 ambapo kwa Unguja wilaya ya Mjini inaongoza kwa asilimia 19.3 ikifuatiwa na wilaya ya Kaskazini B asilimia 15.2, wilaya ya Kati asilimia 10 na Wilaya ya Kusini asilimia 10.5. Kwa upande wa Pemba wilaya inayoongoza ni Chakechake kwa silimia 8.9 ikifuatiwa na Wilaya ya Wete yenye asilimia 7.3.
Utafiti huo ambao unaonyesha idadi kubwa ya wanaoachana kuwa ni vijana wa kati ya umri 19 na 35 umebaini pia kuwa athari zaidi zinazotokana na talaka hizo zinawafikia watoto ambao hunyanyaswa kijinsia,kukosa elimu,kukosa mapezi ya wazazi na matunzo.
Katibu Mkuu alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo yalibaini sababu za kuongezeka kwa talaka kuwa ni pamoja na kutopata matunzo, uke weza, gubu la wakwe, wifi na mashemeji, ukosefu wa elimu ya masuala ya ndoa, kukosekana kwa ushauri nasaha, ufahamu mdogo wa sheria za ndoa, kutokusikiliza ushauri wa wazazi wakati wa kutafuta wachumba.