Na Othman Khamis Ame OMPR
Uongozi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Tanzania umeaswa kuwa na tahadhari na baadhi ya vyama vya siasa vyenye muelekeo wa kuanzisha cheche za kuanzisha vurugu zinazohusishwa zaidi kundi kubwa la Vijana katika sehemu tofauti hapa Nchini.
Tahadhari hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi aliyefika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo miezi michache iliyopita.
Balozi Seif alisema Serikali kupitia vyombo vyake vya dola imekuwa ikiutumia muda wake mwingi kuzuia vurugu na vitendo viovu badala ya nguvu hizo kuzielekeza zaidi katika kuendeleza miradi ya maendeleo, kiuchumi pamoja na ustawi wa Jamii .
Alieleza kwamba Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifikia uwamuzi wa kuwa na mfumo wa Serikali ya umoja wa Kitaifa ili kujaribu kuondosha joto la kisiasa lililokuwa likiikosesha jamii kuwa na muda zaidi wa kufanya shughuli zao za kujitafutia maisha.
Alifahamisha kwamba mfumo huo unaendelea vyema ndani ya Serikali lakini bado hitilafu za migongano inayobeba tuhuma, kashfa na hata matusi inaonekana kuendelea kushamiri nje ya Serikali.
“ Mvutano wa kisiasa uliokuwa ukivukuta ndani ya Visiwa vya Zanzibar kabla na baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vya siasa Nchini Tanzania ulikuwa ukiwanyima fursa ya maendeleo wananchi walio wengi “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alishauri kwamba wakati umefika kwa Taasisi hiyo ya usajili wa vyama vya siasa Nchini kwa kushirikiana na Vyama vya siasa pamoja na jamii yote nchini kujikita zaidi katika kuziunga mkono Serikali kwenye jitihada zao za kulinda na kuimarisha amani iliyopo nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema pamoja na kuhuisha zaidi Demokrasia Nchini lakini bado Uongozi wa Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Nchini unapaswa kuangalia kwa makini masharti yaliyopo ya taratibu za usajili wa vyama vya siasa Nchini ili kuepuka kuwa na utitiri wa vyama visivyokuwa na sifa zinazostahiki kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Alieleza kwamba Demkokrasia halisi iliyotungwa, kuridhiwa na hatimae kukubalika na wananchi walio wengi wakati wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi lazima iheshimiwe, vyenginevyo ni kuelekea kukaribisha vurugu zisizo na msingi wowote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Ofisi hiyo ya Msajili wa Vyama vya vya Siasa kujijengea utaratibu wa kuvihakiki vyama vyote vya siasa Nchini ili kujiridhisha na utendaji wa vyama hivyo.
“ Tumekuwa na vyama vya siasa vipatavyo 21 Nchini Tanzania. Lakini ukifuatilia utendaji wa vyama hivyo unaweza kuvikuta vyengine hata ofisi za kazi Zanzibar havina wakati sheria iko wazi ikisisitiza kwamba Chama chochote cha siasa chenye usajili wa kuudumu lazima kiwe na uwiano wa wanachama Bara na Zanzibar “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Jaji Francis Mutungi kwa kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo wa msajili wa vyama vya siasa Nchini Tanzania na kuahidi kwamba Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itampa ushirikiano wa karibu ili ofisi yake itekeleze majukumu iliyopangiwa.
Alisema Ofisi yake iko wazi muda na wakati wowote ambapo Msajili huyo au ofisa wake yoyote ataona anahitaji msaada wa kiutendaji katika kutekeleza majukumu waliyopangiwa.
Mapema Msajili wa vyama vya Siasa Nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi alisema lengo la Uongozi wa Taasisi yake wakati huu ni kuhubiri amani ili taifa liendelee katika mazingira ya utulivu na amani hasa katika kipindi kijacho cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Jaji Mutungi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kinachohitajika wakati huu ni amani kuliko kitu chengine chochote kwa vile athari ya fujo na vurugu hakuna mwananchi ye yote yule asiyeielewa.
Alisema Ofisi yake imeanzisha utaratibu maalum wa kufanya mikutano ya mara kwa mara kwa kuwashirikisha Viongozi wa Kisiasa wa vyama mbali mbali hasa vile vyenye nguvu katika maeneo husika, watu mashuhuri pamoja na taasisi muhimu katika suala zima la kuhimiza na kusisitiza umuhimu wa taifa kuendelea kuwa na amani.
“ Tunaimani kwamba kwa kutumia njia na utaratibu huu tunaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na nchi itaendelea kubakia kuwa kisiwa cha amani duniani “. Alifafanua msajili huyo wa vyama vya siasa Nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi.
Jaji Francis Mutungi aliteuliwa rasmi na Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Tanzania miezi michache iliyopita na kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo Tarehe 26/8/2013.