STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03 Disemba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wataalamu nchini kutumia lugha nyepesi kuwaelimisha wananchi masuala mbalimbali yanayogusa maisha yao ya kila siku.
Akizungumza katika Kikao cha Kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na robo ya kwanza wa mwaka wa fedha 2013/2014 jana Dk. Shein alisema ni muhimu kwa wataalamu kutumia lugha nyepesi wakati wanapozungumzia masuala yanayohusu wananchi katika maisha yao ya kila siku.
Akitoa mfano wa wataalamu wa kiuchumi, Dk. Shein amesema Serikali imefanya juhudi kubwa na imefanikiwa kukuza uchumi, pato la Taifa, kupunguza mfumuko wa bei na kupunguza umasikini kwa kuimarisha miundombinu na huduma za jamii lakini si wananchi wengi wanaofahamu maana ya kukuwa kwa uchumi.
Amesema wakati umefika kwa wataalamu wa uchumi na mipango kushirikiana na maafisa mawasiliano wa kuandaa mpango maalum utakaohakisha kuwa jamii inaarifiwa ipasavyo kuhusiana na mafanikio na changamoto ambazo Serikali inakabiliana nazo katika kuimarisha hali ya maisha ya wananchi.
“Wataalamu wanapaswa kutumia lugha nyepesi na kutoa mifano ya kawaida wakati wanapozungumzia masuala ya kiuchumi kama kukua kwa uchumi, pato la taifa na mfumuko wa bei”alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa inapaswa kufanyika hivyo kwa masuala yote ya kitaalamu.
Aliipongeza Ofisi hiyo ambayo inajumuisha pia Tume ya Mipango, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa kuongeza ufanisi katika kupanga na kutekeleza majukumu yake kama yalivyooneshwa katika Mpangokazi wake wa mwaka uliopita.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame alisema katika mwaka wa fedha uliopita Ofisi hiyo ilitekeleza majukumu yake kwa wastani wa asilimia 91 na kwa upande wa robo ya kwanza ya mwaka fedha wa 2013/2014 imetekeleza wastani wa asilimia 85.
Alieleza kuwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inatekeleza jumla ya miradi 14 ya maendeleo ikiwemo Mradi wa Kuimarisha Mawasiliano Ikulu, Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini Yenye Kuleta Matokeo ya MKUZA II na Kuratibu Utekelezaji wa MKURABITA
Miradi mingine aliitaja kuwa ni Mradi wa Utafiti wa Hali ya Utumishi nchini, Mradi wa Uimarishaji wa Takwimu nchini, Mradi wa Kuoanisha Masuala ya Idadi ya Watu, Afya ya Uzazi, Jinsia na Umasikini na Kujenga uwezo wa Utekelezaji kwa Taasisi za Serikali.
Kuhusu vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2013/12014 Dk. Mwinyihaji alibainisha masuala nane ambayo wizara hiyo itayasimamia kama vipaumbele ili kufikia malengo ya Wizara.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na kuandaa mikakati itakayohakikisha mazingira ya ukuaji uchumi jumuishi (Inclusive Growth), kuhamasisha ufahamu wa matumizi ya takwimu za Sensa ya Watu na Makazi kwa maendeleo ya nchi, Kuendelea kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Kukamilisha Sera ya Diaspora na Kuzingatia, kusimamia na kuelimisha jamii juu ya misingi ya Utawala bora.
Wakati huo huo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Salum Maulid Salum alikieleza kikao hicho kuwa Ofisi hiyo imefanya mapitio ya Sheria mbili katika mwaka wa fedha uliopita na kuzitaja sheria hizo kuwa ni Sheria Namba5/2003 ya mafao ya Viongozi Maalum na Sheria Namba 1/1980 ya Vyuo vya Mafunzo.
Alieleza pia kuwa Ofisi hiyo imeratibu utafiti juu ya maoni ya wananchi kuhusu huduma na ubora wa taarifa zinazotolewa na Idara ya Mawasiliano Ikulu na imeanza kuyafanyia kazi matokeo ya utafiti huo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.