HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA MAENDELEO YA WANAWAKE NA USTAWI WA JAMII KUHUSIANA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014.
Mheshimiwa Spika
Kila sifa njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu aliyetujaalia afya na uzima, tukaweza kuendelea na majukumu yetu ya kila siku na kuniwezesha kusimama mbele za Baraza lako tukufu kuwasilisha maoni ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii kwa bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Mheshimiwa Spika
Napenda kukushukuru kwa dhati kunipa fursa hii adhimu ya kuwasilisha maoni ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja watendaji wake wote wa Wizara kwa mashirikiano yao katika kipindi chote cha kazi za Kamati.
Mheshimiwa Spika
Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii imekuwa ikifanya kazi zake na Wizara kwa mashirikiano makubwa. Kamati ilipitia Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa umakini na kuishauri Wizara na Serikali kikamilifu.
Mheshimiwa Spika
Baada ya utangulizi, naomba kuanza kutoa maoni ya Kamati katika Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuangalia utekelezaji wa Wizara katika Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu, Idara zake mbali mbali na sehemu nyingine ambazo Kamati zimeona kuna umuhimu mkubwa wa kuzitolea maoni yake.
Mheshimiwa Spika
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu ni chombo muhimu ambacho kina jukumu la kuzikagua skuli zote za Serikali na Binafsi ili kuhakikisha kuwa elimu bora inatolewa kwa mujibu wa mitaala na mihutasari inayokubaliwa na Wizara.
Mheshimiwa Spika
Ubora na mafanikio ya elimu yanategemea sana utendaji nzuri wa Ofisi hii. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la matokeo mabaya ya mitihani kwa wanafunzi wa Zanzibar katika ngazi tofauti hasa hasa ya kidato cha nne. Kamati haifurahishwi na matokeo hayo kwa vile yanatoa taswira kuwa katika muda mfupi ujao nchi yetu itakosa wataalamu mbali mbali, kutokana na wanafunzi wetu wengi kushindwa kufanya vizuri hali inayopelekea wengi wao kushindwa kuendelea na masomo katika ngazi za juu.
Mheshimiwa Spika
Kamati yetu imesikitishwa sana na hali mbaya ya Ofisi za ukaguzi kwa upande wa Unguja na Pemba, kwani majengo hayaridhishi na ni machakavu, finyu na yamekosa rasilimali za kutosha kama vitendea kazi na fedha katika kutekeleza majukumu yao mbali mbali. Mheshimiwa Spika, Wafanyakazi wa ofisi hii ni kama waliotelekezwa katika mazingira yasiyoridhisha na ule umuhimu wa kazi wanazozifanya haulingani na mazingira waliyopo. Hivyo, Kamati inashauri kuboreshwa kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika
Kamati inaishauri Serikali kuipa umuhimu Ofisi hii kwa kuipatia fedha za ruzuku kwa kiwango cha kutosha. Ofisi imekuwa inaongezewa fedha kupitia bajeti ya wizara kwa miaka mitatu mfululizo ambapo bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 iliingiziwa shilingi za kitanzania milioni thamanini (80,000,000), mwaka wa fedha 2012/2013 zilingizwa milioni tisini (90,000,000) na katika mwaka huu wa fedha ruzuku kwa ajili ya uendeshaji zinatarajiwa kuingizwa jumla ya shilingi milioni mia moja na sita (106,000,000). Ongezeko hilo ni faraja kwa Ofisi hii lakini jee ongezeko hilo linaenda sambamba na mahitaji au majukumu ya Ofisi?
Mheshimiwa Spika
Aidha, Kamati inaishauri Wizara kuharakisha matayarisho ya Rasimu ya Uanzishwaji wa Sheria ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu ili kuipa uwezo wa kisheria ofisi hiyo na hatimaye kupata uwezo mkubwa wa kuyafanyia kazi yale mapungufu wanayoyatoa wakaguzi wetu wa elimu katika maskuli.
Mheshimiwa Spika
Bodi ya Huduma za Maktaba
Bodiina jukumu la kuhakikisha kuwa inatoa na kuendeleza huduma za maktaba visiwani Unguja na Pemba. Kamati inaipongeza Bodi kupitia Shirika la Huduma za Maktaba kuimarisha huduma za Maktaba Unguja na kupelekea kuongeza idadi kubwa ya watumiaji wa maktaba hasa baada ya kufunguliwa kwa jengo jipya la Maktaba kuu lilioko Maisara. Hata hivyo bado kuna upungufu wa vitabu vya fani mbali mbali ikiwemo ya sayansi na Kamati inaiagiza uongozi wa maktaba na wizara kuongeza bidii ya kupata vitabu hivyo.
Mheshimiwa Spika
Kamati ina masikitiko makubwa kwa upande wa Pemba, maktaba iliyopo Chake chake ndio maktaba pekee inayotegemewa kwa Pemba mzima na kumekuwa na msongamano mkubwa katika maktaba hiyo kutokana na ufinyu wa nafasi hali inayopelekea kutokuwepo kwa huduma bora kwa watumiaji wa maktaba hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyoWizara kwa upande wa Pemba imejitahidi kupeleka vitabu katika skuli zilizopo vijijini. Kamati yetu inapongeza sana jitihada za Wizara kuweza kupeleka vitabu katika skuli zilizopo vijijini kwa kutumia mpango wa visanduku, mpango huo umesaidia kuwajenga wanafunzi kuwa na tabia ya kupenda kujisomea na Kamati inashauri mpango huo uendelezwe na kuweza kufikishwa katika vijiji mbali mbali.
Mheshimiwa Spika
Kamati inaitaka Serikali kuzingatia na kuipa umuhimu ujenzi wa tawi la maktaba pemba na kuhakikisha kuwa inaitilia Wizara, fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Upanuzi na Uimarishaji wa Huduma za Maktaba. Mradi utekelezaji wake ulianza tangu mwaka wa fedha 2010/2011 na hadi sasa umekuwa unasuasua.Kamati yetu ina hamu kubwa ya kuona ujenzi wa maktaba Pemba unafanyika kupitia mradi huo.
Mheshimiwa Spika Kamati imebaini kuwa skuli nyingi Pemba zimekosa huduma za maktaba, ambapo kwa sasa ni skuli tano mpya na tatu kongwe zina huduma hiyo. Kamati inaishauri Wizara kufanya mpango wa kuanzisha maktaba kwa kila wilaya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za maktaba kwa wananchi wa kisiwa hicho.
Idara ya Elimu ya Maandalizi na Msingi.
Tunaipongeza Serikali yetu kwa kuona umuhimu mkubwa wa kuweka elimu ya maandalizi kuwa elimu rasmi katika mfumo wetu wa elimu Zanzibar na kwa kuzingatia kuwa, elimu ya maandalizi ndio msingi wa kumjenga mtoto kwa ajili ya elimu ya awali.
Mheshimiwa Spika, bado hakuna chuo kinachowaendeleza walimu wa maandalizi katika ngazi ya stash-hada na shahada Zanzibar, hali inayoashiria kuwa, bado Wizara ina jukumu kubwa la kujipanga katika kuendeleza elimu hii kwa kuwaendeleza walimu wake.
Kamati yetu inaishauri Wizara kuipitia Sera yao ya Elimu ili kuweza kuandaa mpango maalum na kamili wa namna ya kuiimarisha na kuwaendeleza walimu wa maandalizi.
Mheshimiwa Spika, Idara pia inaratibu vyuo vya Qur-ani na madrasa lakini mpaka sasa hakuna mtaala unaofahamika katika kutoa mafunzo katika vyuo vya Qur-ani na Madrasa. Kamati yetu inaishauri Wizara ikishirikiana na ofisi ya mufti kuvisamimia vyuo vya Qur-an na madrasa kwa kuwa na muongozo maalum wa kuendesha vyuo vya Qur- ani na pia kuwepo na Utaratibu wa kufanyiwa ukaguzi wa vyuo na kuviandalia mazingira mazuri ya kujisomea.
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni utamaduni wetu wazanzibar kuwapeleka watoto wetu katika vyuo vya Qur-ani kama ni sehemu ya mwanzo ya kujifunza mtoto hata kabla ya kupelekwa katika skuli za maandalizi lakini cha kusikitisha ni kuwa, kutokana na elimu hiyo kutupwa na kudharaulika watoto wamekuwa hawapendi kwenda madrasa kutokana na mazingira mabaya ya vyuo hivyo, Kamati yetu inasisitiza tena kuwepo kwa mazingira bora katika vyuo na madrasa zetu ili kuwatia hamu watoto wetu kusoma elimu ya dini.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya msingi nayo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu. Kamati yetu iliarifiwa kuwa kwa upande wa Pemba shule za Micheweni,Wete,Chakechake na Mkoani zina upungufu mkubwa wa walimu ambao husababishwa na ongezeko kubwa la maskuli majimboni usioenda sambamba na ajira mpya za walimu,walimu wengi wanaostaafu ni wa skuli za msingi,idadi ya wanafunzi kuwa kubwa na walimu wengi wa msingi wanapoenda kuongeza kiwango cha elimu huwa hawapendi kurudi kusomesha skuli za msingi au hukimbilia kada nyengine.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inaiomba Serikali kuisaidia Wizara katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbali mbali zinazoikabili Idara ya Elimu ya Msingi pamoja na kufanya haraka ajira za walimu katika skuli za msingi.
Mheshimiwa Spika.
Kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Wizara.
Wizara imekuwa ikitekeleza miradi mbali mbali kwa ufanisi lakini Kamati imekuwa na masikitiko makubwa juu ya utekelezaji usio wa ufanisi kwa Mradi wa Upanuzi wa Huduma za Maktaba,Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Ufundi na Mradi wa Ujenzi wa Vyuo vya Kiislamu ambapo miradi yote hiyo inatekelezwa na Serikali pekee.
Mheshimiwa Spika.
Katika miradi hiyo Kamati yetu imebaini uingizwaji wa fedha usio wa kuridhisha. Hivyo, Kamati yetu inaitaka Serikali katika bajeti ya mwaka huu wa fedha (2013/2014) kuingizia fedha Wizara ipasavyo ili iweze kutekeleza miradi yake mbali mbali kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika
Elimu Mjumuisho.
Kamati yetu inaipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupitia Kitengo chake cha Elimu Mjumuisho, kuweza kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum ya kielimu, wakiwemo watoto wenye ulemavu na watoto walioko katika mazingira hatarishi katika skuli zilizopo Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo Kamati inaishauri Wizara kuongeza malipo ya motisha ( posho) kwa walimu wanaosomesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwani walimu hao wamekuwa wanafanya kazi ngumu sana kutokana na ukubwa wa madarasa ya wanafunzi hao.
Mheshimiwa Spika, walimu hao ingawa wamekuwa wanapewa motisha kutokana na kazi ngumu wanayoifanya lakini Kamati yetu kwa upande wa Pemba ilibaini kuwa kiwango cha motisha wanayolipwa cha shilingi elfu tano (5000/) katika Skuli za Michakaini na Pandani ni kidogo na cha muda mrefu tokeo mwaka 1991. Kiukweli hakilingani na ugumu wa kazi pamoja na mabadiliko ya gharama za maisha, hivyo Kamati inaishauri Wizara kufikiria kuwaongezea kiwango ili kuwapa moyo kutokana na kazi ngumu na ya thamani wanayoifanya.
HITIMISHO:
Sekta ya Elimu ni sekta muhimu ambapo kuboreshwa kwa sekta hii kutapelekea mafanikio ya sekta nyenginezo. Kamati yetu imegundua changamoto nyingi katika sekta hii muhimu ikiwemo kutopewa kipao mbele kwa watumishi wake. Taaluma ya elimu bado haijapewa kipaumbele, walimu wetu wamekosa chombo huru cha Sheria ambacho kitaweza kusimamia maadili na taaluma ya ualimu.
Aidha, walimu wetu wamekuwa na maslahi duni na ualimu umekuwa unashuka hadhi yake. Kamati yetu inaiomba Serikali kusimamia sekta ya Elimu ipasavyo pamajo na kuwepo chombo huru cha kusimamia maslahi yao ili tuone hadhi ya elimu inarudi tena Zanzibar.
Mheshimiwa Spika
Baada ya maoni hayo ya Kamati, sasa napenda kuwatambulisha wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii kama ifuatavyo:-
1. Mhe. Mgeni Hassan Juma Mwenyekiti
2. Mhe. Hassan Hamad Omar Makamo Mwenyekiti
3. Mhe. Ali Salum Haji Mjumbe
4. Mhe. Abdi Mosi Kombo Mjumbe
5. Mhe. Farida Amour Mohamed Mjumbe
6. Mhe. Mwanaid Kassim Mussa Mjumbe
7. Mhe. Mohammed Mbwana Hamad Mjumbe
Nachukua fursa hii kuwapongeza sana wajumbe wa Kamati na kuwaomba kuendelea na kujituma katika kuendeleza majukumu yetu. Pia nawapongeza makatibu wetu wawili wa Kamati ambao wamekuwa wakitusaidia kwa karibu katika kutekeleza kazi zetu. Nao ni:-
1. Ndg. Maryam Rashid Ali Katibu
2. Ndg. Asha Said Mohamed Katibu
Mheshimiwa Spika naunga mkono hoja hii mimi binafsi na kwa niaba ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii tunaunga mkono hoja.
Ahsante sana kwa kunisikiliza na naomba kuwasilisha.
Ahsante.
…………..
Mhe. Mgeni Hassan Juma,
Mwenyekiti,
Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.