Na Ussi Talib
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba Wilaya ya Kati Unguja, wamependekeza Katiba ijayo itamke rasmi kuwa mshirika wa Muungano ni Tanganyika na siyo Tanzania bara.
Maoni hayo yalitolewa jana huko Dunga wilayani humo mbele ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania inayongozwa na Mwenyekiti,Awadhi Ali Said.
Makame Ali Makame,alisema ikiwa Tanzania imekusudia kuondoa kero za muungano basi irudi katika uasilia wake wa nchi mbili huru zilizoungana ambazo ni Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar.
“Sawa na kukubaliana na mfumo mpya wa Muungano lakini Zanzibar iitwe hivyo na Tanganyika iitwe hivyo kama ilivyokuwa zamani” alisema Makame.
Pia aliitaka rasimu kila sehemu inayotaja Tanzania Bara itamke Tanganyika kwani kuweka kinyume na hivyo ni kumpa nafasi mmoja kujiona mkubwa.
Abuubakar Ussi Fadhili yeye alisema ni vyema kuweka uwazi huo ili kuondoa matatizo ambayo yanaweza kujitokeza.
Sambamba na hilo kwa upande wa Amin Yusouf Mussa mambo ya muungano yamependekezwa kuwa saba.
“Leo tunapendekeza mambo saba ya Muungano lakini Tanganyika haipo kama ikija kuyataka itakuwaje?”alihoji Mussa.
Akitoa ufafanuzi Mwenyekiti wa Kamati ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Zanzibar,Awadhi Ali Said alisema,ili yatekelezeke hayo tume itaweka wazi shughuli za upande wa Tanzania bara ambazo zilikuwa zinashughulikiwa na Serikali ya Muungano na kuunda chombo chake kuyashughulikia.
Wajumbe hao wa Kamati ya mabadiliko ya Rasimu ya Katiba Mpya, wametawanyika katika sehemu mbalimbali kwa lengo la kukutana na wajumbe wa mabaraza ya Katiba walioteuliwa kuwakilisha wananchi ili kuunda Katiba Mpya itakayoleta mabadiliko ya mfumo na muundo mzima wa uongozi, watu na mamlaka husika kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Chanzo - Mwananchi