HOTUBA YA MHE. BALOZI SEIF A. IDDI, MAKAMU WA PILI WA RAIS KATIKA UFUNGUZI WA CHUMBA CHA CHINI YA BAHARI “THE MANTA UNDERWATER ROOM” KATIKA HOTELI YA MANTA RESORT, MAKANGALE - PEMBA
Mheshimiwa Said Ali Mbarouk, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo,
Mheshimiwa Bihindi Hamad Khamis, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo,
Bwana Mathew Saus, Mkurugenzi Mtendaji – The Manta Resort,
Mheshimiwa Dadi Faki Dadi, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, Pemba.
Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo,
Dkt. Ahmada Khatib, Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Utalii,
Ndugu Saleh Ramadhan Ferouz, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii,
Viongozi mbali mbali wa Serikali,
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana.
Asaalam Aleykum,
Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kukutanisha hapa tukiwa wazima na wenye afya njema tukiwa katika shamra shamra za kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Aidha, napenda kuushukuru sana uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kunihusisha kwao kuwa pamoja nanyi nikiwa mgeni rasmi katika shughuli hii muhimu ya kihistoria nchini mwetu.
Ndugu Wananchi,
Leo ni siku muhimu sana katika maendeleo ya Sekta ya Utalii hapa Zanzibar kutokana na ufunguzi wa chumba hichi maalum cha kulala wageni kilicho chini ya bahari. Uwepo wa chumba hichi ni kielelezo muhimu katika kukuza utalii hapa Zanzibar kwani ni moja ya kivutio pekee kwa wageni watakaobahatika kukaa katika chumba hiki.
Ndugu Wananchi,
The underwater room ambacho kiko umbali wa mita 4 kutoka chini ya bahari kitatoa fursa kwa wageni kuweza kupata sehemu maalum ya kuota jua (sunbathing on top deck), kupata sehemu maalum ya chakula, vinywaji pamoja na kulala huko chini ya bahari akiangalia maumbile ya viumbe mbali mbali vilivyoko chini ya bahari (tropical marine environments).
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuupongeza Uongozi wa Manta Resort kwa kuamua kuwekeza katika mradi huu wa kipekee nchini mwetu. Ni matumaini yangu mradi huu utaweza kuitangaza vizuri Zanzibar duniani kote.
Ndugu Wananchi,
Nchi chache sana duniani zina mfano wa hoteli kama hii. Nchi ambazo zina aina ya chumba kama hiki kwa mujibu wa taarifa nilizonazo ni:-
1. Jules Undersea Lodge iko Puerto Rico, imetengenezwa mwaka 1970.
2. Utter In (Otter) iko Vasteras Sweden, imetengenezwa mwaka 2000.
3. Crescent Hydropolis iko Dubai, ambayo iko katika matengenezo itakuwa na vyumba 220.
4. Poseidon Undersea Resort, iko Fiji, imefunguliwa mwaka 2009.
Ndugu Wananchi,
Kwa kuwa aina ya hoteli hizi ni chache sana duniani, ni dhahiri kama nilivyosema awali Zanzibar nayo itakuwa katika ramani ya dunia katika utalii kuwa na hoteli kama hii katika nchi za Afrika.
Ni matumaini yangu Uongozi wa hoteli utatoa huduma bora na za uhakika ili kuongeza idadi ya watalii kutembelea Pemba.
Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwapa mashirikiano ya karibu wawekezaji wa sekta ya utalii ili kuweza kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.
Ndugu Wananchi,
Sisi Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais na mimi mwenyewe tunapofanya ziara nchi za nje huwa tunawabembeleza wawekezaji wa nchi hizo kuja kuwekeza nchini mwetu hasa katika sekta hii ya utalii na sekta ya viwanda. Bahati nzuri huwa wanatuitikia na wanakuja na ndiyo maana leo Zanzibar ina mahoteli mazuri mazuri nchini mote, Mikoa ya Kaskazini na Kusini Unguja. Katika Mkoa wa Mjini na Magharibi, karibu tutashuhudia ufunguzi wa hoteli nyengine ya aina yake katika Mji Mkongwe, katika eneo lililokuwa Mambo Msiige. Kwa ufupi mpaka sasa, Zanzibar imeweza kuongeza idadi kubwa ya mahoteli ya kulala wageni kwa mfano:
Hoteli zenye hadhi ya nyota 5 ziko 26, nyota 4 ni 21, nyota 3 ni 26, nyota 2 ni 18 na nyota 1 ni 61.
Ndugu Wananchi,
Vile vile, takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2012/2013 idadi ya watalii waliofika Zanzibar ilipungua sana kutoka watalii 392,481 na kufikia watalii 274,261 sawa na upungufu wa asilimia 118,220. Hata hivyo, pamoja na upungufu huo, kulikuwa na ongezeko kubwa la makusanyo kwani jumla ya Shilingi 41,811,962,911.62 zilipatiana ikilinganishwa na Shilingi 34,597,281,778.74 za mwaka 2011/2012. Ongezeko halisi lilikuwa Shilingi 7,214,681,133.18.
Ndugu Wananchi,
Hali hii ya kuongezeka makusanyo licha ya kupungua sana kwa idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2012/2013 inatokana na sababu mbali mbali ikiwemo kupanda na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania, aina ya watalii wanaokuja Zanzibar na kuzibwa kwa mianya kwenye vianzio vya mapato.
Haya ni mafanikio makubwa tuliyoyapata katika sekta hii ya utalii.
Lakini pamoja na maendeleo hayo ya ujenzi wa mahoteli hayo, tutahitaji watalii waje kukaa katika mahoteli hayo na kutumia fedha zao za kigeni nchini mwetu ambazo zinakuwa sehemu ya pato la Taifa. Hata hivyo, wageni hao hawatakuja kama hatutoendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu. Wageni wanakuja nchini mwetu kubadilisha hali ya hewa na kuona mazingira mapya.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na hali hiyo, hatuna budi sote kwa pamoja kupania kuiweka nchi yetu katika hali ya amani na usalama ili wageni wetu wakija waweze kukaa bila ya wasiwasi. Tuwe wanyenyekevu kwa wageni wetu, tuwaonyeshe bashasha za Kizanzibari kama ilivyo tabia yetu, tusiwabughudhi wakiwa fukweni au katika matembezi yao. Tunataka wafurahie ukaazi wao katika Visiwa vyetu vya karafuu na spices.
Ndugu Wananchi,
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, sina budi kuchukua nafasi hii tena kuushukuru Uongozi wa Manta Resort kwa kuwekeza mradi huu muhimu wa utalii hapa Pemba.
Vile vile kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa chumba hichi maalum cha chini ya bahari ikiwa ni muendelezo wa Sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Baada ya maelezo hayo, sasa kwa heshima naomba kutamka rasmi kwamba chumba cha kulala wageni cha chini ya bahari nimekifungua rasmi.
Ahsanteni sana.