Na Khadija Khamis Maelezo
Imeelezwa kuwa iko haja ya Serikali kuandaa mitaala ya pamoja katika Skuli za maandalizi ili kuepuka kutofautiana kiuwezo wa elimu kwa wanafunzi wa Skuli za Serikali na Skuli za Kibinafsi.
Wamesema elimu ya maandalizi ni msingi wa kumuezesha mtoto kujiandaa ili akianza elimu ya msingi aweze kuwa na ufahamu mzuri .
Wajumbe wa baraza la wawakilishi wameeleza hayo wakati wakichangia Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo na mji wa Zanzibar .
Aidha wawakilishi hao walisema pamoja na mitaala ya masomo pia wameishauri Wizara ya elimu kuandaa mitaala ya michezo ili kuweza kukuza kiwango cha michezo nchini.
Wakizungumzia suala la hatimiliki, wachangiaji hao walisema kuna skuli nyingi za Unguja na Pemba hazina hatimiliki licha ya kwamba baadhi ya skuli hizo zina umri wa miaka mingi .
Aidha walisema kuwa iko haja ya kuandaliwa vifaa kwa ajili ya elimu mjumuisho na walimu wanaosomesha masomo hayo waangaliwe kwa maslahi kwani wanakabiliana na kazi ya ziada katika kufundisha wanafunzi hao .
Aidha walisema Wizara ya Elimu imeajiri walimu 578 katika kipindi cha mwaka huu lakini hadi sasa walimu waliomaliza mwaka 2008 hawajapata ajira .
Wakieleza changamoto zilizojitokeza ni ukosefu wa walimu katika wilaya za Pemba. Wete.Chakechake na mkoani .
Wakifahamisha kwamba walimu wanaopata ajira wazingatiwe na wilaya zao wanazoishi kwa kurahisishiwa masafa.
Aidha walieleza kuwa walimu hawafanani na chochote hivyo wanahitaji kuenziwa kutunzwa na kuthaminiwa.