Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Hotuba ya Ufungaji Kikao cha 14 cha Baraza la Wawakilishi leo

$
0
0
HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF A. IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI NA NNE WA BARAZA LA
WAWAKILISHI ZANZIBAR, TAREHE 20 DISEMBA, 2013

1.     Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uzima, afya njema na utulivu na pia kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu tuliyojipangia katika Mkutano huu wa Kumi na Nne  kwa salama na amani. Pili, nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Wasaidizi wako wote kwa umakini, busara na hekma zilizopelekea kuendesha Mkutano huu wa Baraza la Wawakilishi kwa ufanisi mkubwa sana.

2.     Mheshimiwa Spika, vile vilenapenda niwashukuru Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Baraza kwa kuziongoza Kamati zao na kutekeleza majukumu yaovyema.

3.     Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa nimpongeze Rais wa Zanzibarna Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza nchi yetu kwa umakini na kuweza kupata mafanikio makubwa. Ushauri na miongozo yake kwetu inatusaidia sanakatika kutekeleza majukumu yetu, kwa manufaa ya nchi yetu na wananchi wote.

4.     Mheshimiwa Spika, aidha, nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu kwa majadiliano mazuri na ushauri wenye kujaa busara na hekima wenye nia ya kuimarisha utendaji na utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku. Pia, napenda kuwashukuru sanaWaheshimiwa Mawaziri kwa kutoa ufafanuzi wa kina wa hoja mbali mbali zilizoulizwa na Waheshimiwa Wawakilishi kwenye mkutano huu.

5.     Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 5 Disemba, 2013 Bara letu la Afrika na ulimwengu kwa jumla ulipata msiba mkubwa na usioweza kusahaulika wa kuondokewa na kiongozi shupavu, mvumilivu na mtetezi wa haki za binaadamu wote na mkombozi wa wananchi wa Afrika ya Kusini,  Mheshimiwa Mzee Nelson Mandela. Ni wazi kwamba kiongozi huyu aliepigania uhuru katika nchi yake ya Afrika Kusini hatosahaulika kwa kuionesha dunia utu wa hali ya juu kwa kuweza kusamehe na kusahau yaliyopita na kuwataka wananchi wote wa Afrika Kusini kushirikiana bila ya ubaguzi wa dini, rangi au ukabila.  Mzee Mandela hakuwa mtu wa kulipa kisasi kamawengi wangeweza kufikiria.  Mzee Mandela ameutumia umri wake wote wa ujanani jela ambako amefungwa kwa muda wa miaka 27.

6.     Mheshimiwa Spika, bila shaka tuna mengi ya kujifunza kutokana na maisha ya Mzee Nelson Mandela katika kujali utu, kusamehe, uvumilivu na moyo wa kuipenda nchi na Bara letu na kuwa na mahusiano mema na binaadamu wote katika dunia.  Mzee Mandela aliwasamehe waliomfanyia uovu huo, pamoja na kuamini kuwa Mungu hakumuumba mtu muovu ila uovu ni wa mtu mwenyewe.


7.      Mheshimiwa Spika, kama sote tunavyoelewa kwamba, kila ifikapo tarehe 12 Januari ya kila mwaka, nchi yetu inaadhimisha sherehe za Mapinduzi yetu Matukufu yaliyotokea mwaka 1964. Ifikapo tarehe 12 Januari, 2014 Mapinduzi hayo yatatimiza miaka 50.

8.     Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Maadhimisho haya yaliyozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 15 Agosti, 2013 yanaendelea vizuri. Tangu yalipozinduliwa tumeshuhudia wananchi wakisherehekea kwa kufanya usafi wa mazingira, kushiriki katika matamasha mbali mbali ya michezo na burudani pamoja na  uzinduzi, uwekaji wa mawe ya msingi na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo. Nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wazidi kuhamasisha wananchi kuendelea kushiriki kwa wingi katika matukio mbali ya sherehe hizi pamoja na siku ya kilele hapo Uwanja wa Amaan, tarehe 12 Januari, 2014. 

Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote waliopangiwa kuzindua au kuweka mawe ya msingi kwa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa kuifanya kazi hiyo vizuri na kwa ufanisi.

9.     Mheshimiwa Spika, katika kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, Serikali imeandaa maonesho yatakayofanyika katika viwanja vya Beit al Ras kwa siku nne kuanzia tarehe   2 Januari, 2014 hadi tarehe 5 Januari, 2014 ambapo Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi na Jumuia za Kiraia watapata fursa ya kuonesha shughuli zao wanazozifanya, huduma wanazozitoa au bidhaa wanazozalisha. Hii ni fursa ya pekee kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na wageni kutembelea kwenye maonesho haya ili kuona mafanikio yetu ya miaka 50 tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

10.Mheshimiwa Spika, sotetunaelewa kwamba Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Awamu ya Tatu (TASAF III) tayari umeshaanza shughuli zake hapa Zanzibarna imeshafanya shughuli nyingi zikiwemo kutoa mafunzo ili kujenga uelewa wa lengo la TASAF Awamu ya Tatu kwa wadau mbali mbali tukiwemo Waheshimiwa Wawakilishi wa Baraza lako tukufu. Aidha, kaya maskini tayari zimeanza kutambuliwa kwa mashirikiano na wanajamii wenyewe. Kwa Unguja jumla ya kaya maskini 2,500 zimetambuliwa na kwa Pemba hadi sasa jumla ya kaya 4,000 zimeshatambuliwa. Kazi ya kuzitambua kaya maskini inaendelea kwa Shehia zote za Unguja na Pemba. Aidha, hatua ya kuzihakiki kaya zilizokwisha tambuliwa zimeanza na tunatarajia kuanza kutoa malipo kwa kaya hizo ifikapo mwezi Januari, 2014. Nachukua nafasi hii, kuwaomba Waheshimiwa Wawakilishi kuendelea kutoa ushirikiano katika zoezi zima la kuzitambua na kuzihakiki kaya maskini ili malipo yaweze kufanyika kwa wale wanaostahiki na si vyenginevyo. 

11.                    Mheshimiwa Spika, bado tumo katika kipindi cha mvua za vuli na katika kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia kupatikana kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake kuikumba dunia, ni vyema kwa taasisi zote zinazohusika kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa na kutoa taarifa za mapema kwa wananchi hususan wakulima na wavuvi na wanaosafiri kwa kutumia usafiri wa angani na baharini ili kuchukua tahadhari na kupanga vyema shughuli zao.

12.                    Mheshimiwa Spika, Sekta za Kilimo na Maliasili bado zinaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja katika kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za wananchi walio wengi vijijini na mijini.  Kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sekta hizi zilichangia asilimia 30.2 ya pato la Taifa na inakadiriwa  kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hii kwa kuwapatia ajira na mapato.
13.                    Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza azma yake ya kuleta Mapinduzi ya kilimo nchini Wizara  imeweza kufanikisha mambo yafuatayo:-
Serikali ya Awamu ya Sabakwa kupitia na Wizara ya Kilimo na Maliasili itaendelea kulipa kipaumbele suala la kuwapatia wakulima ruzuku kwenye nyenzo na pembejeo za kisasa (mbegu bora, mbolea, dawa na huduma za matrekta) ili kuinua uzalishaji hasa kwa mazao ya chakula ikiwemo mpunga na mboga mboga. Aidha, katika kipindi cha misimu ya kilimo 2010 hadi 2013 kumekuwa na ongezeko maradufu la ununuzi na matumizi ya pembejeo hizo kama ifuatavyo:-
Kwa mbegu bora, Serikali imeongeza pembejeo kutoka tani 55 mwaka 2010 na idadi hiyo kuongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia tani 620 mwaka 2013, mbolea – TSP na Urea kutoka tani 130 mwaka 2010 hadi kufikia tani 1,500 mwaka 2013 na dawa ya magugu kutoka lita 12,000 mwaka 2010 hadi kufikia lita 30,000 mwaka huu.
Kwa upande wa matrekta Wizara ya Kilimo na Maliasili inatarajia kuingiza nchini matreka 20 kutoka Suma JKT ya Tanzania Bara hivi karibuni.

Mambo Yaliyojitokeza Barazani:

14.   Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 57 ya msingi na maswali kadha ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wajumbe na kupatiwa majibu na ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri.

Nawapongeza kwa dhati Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu kwa kuuliza maswali hayo ambayo yalikuwa na lengo la kuwaelimisha wananchi.

Aidha, Waheshimiwa Wajumbe walijadili na kupitisha jumla ya Miswada mitatu ambayo ni:-

a)     Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Baraza la Vijana la Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo;
b)     Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Amri ya Barabara, Sura 134 na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo;
c)      Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti ya Kukinga na Kusimamia Maswala ya UKIMWI Zanzibar, Kulinda na Kuendeleza Haki za Watu Wanaoishi au Walioathirika na Virusi vya UKIMWI na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.


15.   Mheshimiwa Spika, Mswada wa Kwanza uliowasilishwa kwenye Baraza lako Tukufu na kujadiliwa ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Baraza la Vijana la Zanzibarna Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Kuwasilishwa kwa mswada huu kunatokana na kilio cha siku nyingi cha vijana wetu wa Zanzibar kutaka kuwa na chombo chao kilichoanzishwa kisheria cha kuwaunganisha na kufuatilia masuala mbali mbali yanayowahusu na ya maendeleo kwa nchi yetu.

16.   Mheshimiwa Spika, madhumuni makubwa ya Mswada huu ni kuwakuza vijana wetu ili wawe wazalendo kwa Taifa lao kwa kuwajenga ili wajitambue, wajiheshimu wao na waheshimu wengine na pia kuitambua kwa kina jamii yao kisiasa na kiuchumi na pia kuuthamini utamaduni wa nchi yao. Aidha, Mswada huu una lengo la kuwaweka pamoja vijana wetu na kuweza kubadilishana mawazo ambayo yatawasaidia wao pamoja na kulisaidia Taifa letu ili liendelee kusonga mbele. Taifa lenye nguvu kazi imara ambayo ni vijana linapata maendeleo kwa kasi sana. Hivyo, nasi hatuna budi kuwakuza vijana wetu kwenye mtazamo wa kizalendo na kimaendeleo ili kuisaidia nchi yetu.

17.   Mheshimiwa Spika, Mswada mwengine uliowasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na Wajumbe ni Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Amri ya Barabara, Sura 134 na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Mswada huu una lengo la kurekebisha Sheria ya Barabara Sura 134 ambapo vifungu vingi vilivyomo kwenye sheria hii haviwezi kufanya kazi kwa wakati tulionao kutokana na kuwa Sheria hii ni ya muda mrefu na baadhi ya vifungu haviendi sambamba na mabadiliko yaliopo ya ufanyaji kazi.

18.   Mheshimiwa Spika, Mswada wa mwisho uliowasilishwa ni Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti ya Kukinga na Kusimamia Masuala ya UKIMWI Zanzibar, Kulinda na Kuendeleza Haki za Watu Wanaoishi au Walioathirika na Virusi vya UKIMWI na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Mswada huu una madhumuni ya kuweka mfumo wa kisheria wa kuzuia na kusimamia masuala yote ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI hapa Zanzibar kwa lengo la kuimarisha haki za binaadamu kwa wale wote wanaoishi au walioathirika na virusi vya UKIMWI. Aidha, kuwepo kwa Mswada huu kutasaidia sanakuweka uratibu mzuri wa masuala yanayohusiana na UKIMWI na Virusi vya UKIMWI kwa Taasisi na Jumuiya zote zinazojishughulisha na masuala haya. Pia, Mheshimiwa Spika, Mswada huu umetoa wajibu wa kila mmoja wetu kuweza kujua hali yake ya Virusi vya UKIMWI kwa kupima afya yake na vile vile kuweza kujilinda yeye mwenyewe na kuwalinda wengine kutokana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.   Mswada unasisitiza jamii kujiepusha na mila na itikadi potofu pamoja na mazoea ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababisha kuenea kwa Virusi vya UKIMWI. Ni busara sisi Waheshimiwa Wawakilishi pamoja na wananchi wote tukazingatia sanaelimu tunayopata inayohusiana na masuala yote ya UKIMWI ikiwemo masuala ya kinga, maambukizi, huduma na mengineyo. Sote tunaelewa kwamba UKIMWI ni ugonjwa hatari na matibabu yake hadi sasa hayajapatikana. Hivyo, ni bora zaidi kujikinga.  Tusidanganywe na watu wanaojidai madaktari wa dawa asilia na wanaweza kulitibu gonjwa hili.  Si kweli bado dawa ya aina yoyote haijapatikana pamoja na utafiti wote unaofanyika kuipata dawa ya kuponyesha ugonjwa huu.


19.   Mheshimiwa Spika, Baraza lako Tukufu pia lilipata nafasi ya kujadili kwa kina Ripoti ya Kamati Teule ya Kushughulikia Migogoro ya Ardhi ambayo Mwenyekiti wake alikuwa ni Mheshimiwa Ali Mzee Ali. Nachukua nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati hii pamoja na Wajumbe wake wote kwa kuifanya kazi hii na kuikamilisha na kuwasilisha ripoti yake. Nilihakikishie Baraza lako Tukufu kuwa Serikali imeipokea ripoti hii na itaifanyia kazi ipasavyo.  Hata hivyo, ripoti hii imekuja kinyume na matarajio ya wengi, pamoja na baadhi ya Wajumbe wenyewe.  Maeneo mengi yenye migogoro na malalamiko yameachwa bila ya kuchunguzwa.  Muda ambao Kamati hii iliyochukua ilitegemewa ingekuja na ripoti nzuri zaidi.  Serikali itaendelea kushughulikia ile migogoro ambayo haikuzingatiwa na Kamati hii na hatua muafaka kuchukuliwa.

20.   Mheshimiwa Spika, Serikali imeyapokea mapendekezo yote yaliomo ndani ya Ripoti ya Kamati na hasa lile linalohusu wananchi kuelimishwa juu ya dhana nzima ya ardhi kuwa mali ya Serikali.  Tunakubaliana na pendekezo hili kuwa ipo haja ya kufanya hivyo na Serikali itaendelea kuwaelimisha wananchi ili waielewe vema dhana hiyo.  Nawaomba Waheshimiwa Wawakilishi washirikiane na Serikali katika kutoa elimu hiyo kwa wananchi wao Majimboni. 

Mheshimiwa Spika, pamoja na kulipokea pendekezo hili, Serikali pia imeyapokea mapendekezo mengine yote na itayafanyia kazi kadri itakavyoona inafaa.

21.   Mheshimiwa Spika, Pia Baraza lako lilipokea hoja mbili za Wajumbe wa Baraza hili zilizowasilishwa na Mhe. Hamza Hassan Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura na Mhe. Mgeni Hassan Juma, Mwakilishi Viti Maalum. Hoja hizo ni:-

a)     Hoja ya Mjumbe ya Kuomba ridhaa ya Baraza kwa ajili ya Kuwasilisha Mswada wa Sheria ya Utawala wa Baraza; na
b)     Hoja ya Mjumbe ya kuliomba Baraza Kutoa Azimio dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto, Zanzibar.

22.    Mheshimiwa Spika, hoja zote hizo zilipokelewa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu.

23.    Mheshimiwa Spika, hoja inayohusu Azimio dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto ilipata michango mingi kutoka kwa Wajumbe wa Baraza lako, na kwa kweli ilistahili kupata michango hiyo kwani suala la udhalilishaji wa watoto ni jambo baya na la kukera sana na linatia aibu nchi.  Na ndiyo maana Wajumbe waliichangia hoja hii kwa uchungu sana. Naviomba vyombo vya sheria vitende haki kwa kuwachukulia hatua kali wale wote watakaothibitika kufanya vitendo hivyo, imetolewa hapa na Waheshimiwa Wajumbe, mifano mingi mingine ni ya aibu na ya kutisha.  Hatuwezi kuvumilia kuwa na watu wa aina hiyo ndani ya jamii yetu.  Napenda nimpongeze sana Mjumbe aliyetuletea hoja hiyo hapa Barazani.


24.    Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena nichukue nafasi hii kukupongeza tena wewe binafsi, wasaidizi wako pamoja na watendaji wote wa Baraza kwa kuhakikisha kwamba shughuli za Baraza zilizopangwa zote zinatekelezwa chini ya maelekezo na busara zako Mheshimiwa Spika.

25.    Mheshimiwa Spika, vile vile niwashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili kwa jinsi wanavyojadili hoja mbali mbali zinazowasilishwa kwenye Baraza kwa umakini wa hali ya juu. Michango na hoja wanazoziibua zinatusaidia kuweza kufanya kazi kwa upeo mkubwa.

26.    Mheshimiwa Spika, Mwisho kabisa navishukuru vyombo mbali mbali vya habari, radio, television na magazeti kwa kuwa nasi kwa kipindi chote cha Baraza hili.  Pia nawashukuru, wakalimani wa alama kwa kazi yao nzuri waliyoifanya ya kuwawezesha wananchi wenye ulemavu wa kusikia kujua nini kilichokuwa kinaendelea ndani ya Baraza hili.

Pia, nawashukuru Wajumbe wote kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa utulivu na umakini mkubwa kwa muda wote wa Baraza hili.  Ninawatakia safari ya salama kurudi Majimboni mwao kuwatumikia wananchi wao.

27.    Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi tarehe 22 Januari, 2014 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.



Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>