HOTUBA YA MHE. MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA MKUTANO MKUU WA JUMUIYA YA WALIMU WAKUU WA SKULI ZA SEKONDARI , ZANZIBAR TAREHE 18 DISEMBA, 2013 SKULI YA SEKONDARI YA LUMUMBA
Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi,
Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu,
Wakurugenzi,
Viongozi mbali mbali wa Vyama na Serikali,
Walimu Wakuu,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Asaalam Aleykum,
Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya njema na tukaweza kukutana hapa, pia kumtakia rehma Mtume wetu Muhammad (S.A.W) katika Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari, Zanzibar (JUWASEZA).
Nashukuru pia kwa kunialika katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza tukiwa tupo katika shamra shamra za kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari, 1964. Miaka 50 inatupa nafasi ya kutafakari na kutathmini maendeleo yetu. Malengo ya Mapinduzi yaliangalia na yanaendelea kuangalia maeneo matatu makuu:
Jambo la Kwanza - kumkomboa Mzanzibari kutokana na ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo, kuondoa matabaka ya Mabwana na Watwana.
Jambo la Pili - Kuleta, kudumisha na kuendeleza maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Kuweza kupambana na adui ujinga na maradhi. Mapinduzi haya Matukufu ya miaka 50 yanakwenda sambamba na miaka 50 ya Elimu Bila ya Malipo. Kwa sasa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ipo katika utekelezaji wa sera mpya ya Elimu ya mwaka 2006. Lengo la sera hiyo ni kuweza kukabiliana na kasi ya maendeleo ya dunia, maendeleo ya dunia, maendeleo ya teknolojia kimazingira na kisaikolojia katika kumuandaa mtoto.
Baada ya miaka 50 ya Mapinduzi, Wazanzibari tumeweza na Serikali yenu imeandaa mwelekeo utakaoinua vipaji vya vijana wetu ambavyo tumeviwekeza katika sera mpya, ufundishaji wa leo ni ule wa kuzingatia ukuzaji stadi mbali mbali za mashi, kama vile za kutatua changamoto tulizonazo, kutunza mazingira, kujieleza, kujitambua na kujitathmini. Mkiwa katika Mkutano Mkuu ni nafasi pekee ya kutafakari mambo mawili muhimu ambayo ni kujitambua na kujithathmini.
Kujitambua ni hali ya kujielewa wewe ni nani, una malengo gani kwa nchi yako na utaifanyia nini katika kuyaenzi Mapinduzi na maendeleo yaliyopatikana.
Kujitathmini ni hali ya kutathmini na kuchukua hatua na kulinda utu wako na nchi yako. Mtu anayejitathmini ndiye anaekuwa muumini mwema na raia mwema, ambae anapambana na kila vitendo viovu na vibaya kama vya unyanyasaji, uhalifu, ubadhirifu na kadhalika.
Jambo la tatu – kumkomboa Mzanzibari kutokana na husda, choyo, chuki na kuweza kuleta mahusiano na muamala mwema, ndio maana tunasema Mapinduzi Daima kwani maneno hayo ndio hazina ya Mzanzibari na hakuna mbadala wa hayo.
Ndugu Walimu Wakuu, nakupongezeni sana Walimu Wakuu kwa uamuzi wenu wa kuunda Jumuiya. Waswahili wanasemao “Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu”. Naamini Jumuiya hii itakuwa chachu ya maendeleo yenu kielimu na kimaisha kwa jumla.
Walimu Wakuu baada ya mkutano huu natumai mtapanga na kuweka maazimio. Matarajio yangu ni kuwa mtapanga mipango bora itakayozingatia mambo yafuatayo:-
· Kuinua viwango vya upasishaji kwa wanafunzi wetu;
· Kuwa na uongozi bora ambao utashirikiana na jamii katika kuziendeleza skuli zetu;
· Kuisaidia Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhusu utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu;
· Kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
· Kulinda na kuimarisha mazingira ya skuli, ili skuli zote ziwe na mazingira rafiki kwa watu wote wanaotumia skuli hizo.
Ndugu Walimu Wakuu, naomba kuchukua nafasi hii kuzipongeza skuli binafsi kwa msaada mkubwa wanaoutoa kwa Serikali yenu kwa kutoa elimu bora bila ubaguzi wowote. Skuli hizi zimeisaidia Serikali kuwapatia ajira raia wa nchi hii, aidha imeipunguzia Serikali mzigo wa kurundikana kwa wanafunzi katika skuli zetu. Natoa wito kwa zile skuli binafsi ambazo bado hazijajiunga kushirikiana na Jumuiya hii kwani ndio itakayokusaidieni kueleza na kutatua changamoto zenu.
Ushauri wangu kwenu:
- Nawaomba kusimamia majukumu ya kazi za kila siku kwa walimu na wanafunzi ili kuinua kiwango cha elimu.
- Kusimamia skuli na mazingira yake ili kuboresha mazingira.
- Kujiendeleza kielimu ili kwenda sambamba na sayansi na teknolojia.
- Kutafuta mahusiano na Jumuiya za nje ili muweze kubadilishana ujuzi na uzoefu.
- Nakuombeni mfanye uchaguzi wa huru na haki ili kuweza kuchagua viongozi bora ambao wataipatia mafanikio.
Mnataka kufanya uchaguzi wa uongozi, hivyo ni jambo la lazima kwa kila mmoja wenu kuwa tayari na yafuatayo:-
- Kupokea matokeo kwani hiyo ndio demokrasia;
- Kuwa tayari kuongoza na kuongozwa kwa mujibu wa Katiba na taratibu zilizopo.
- Kuwa na ari kwa viongozi na wanachama kuhusu utekelezaji wa malengo ya Jumuiya.
- Kuhubiri umoja, mshikamano, amani na utulivu tokea katika ngazi ya Jumuiya ili iwe kigezo kwa Taifa na jamii kwa ujumla.
Ndugu Walimu Wakuu, Kiongozi mzuri ni yule ambaye anafahamu na anathamini kwa vitendo kwamba uongozi ni dhamana inayohitaji uwazi, uadilifu na ukweli, ili kujenga imani kwa unaowaongoza. Unapojenga imani kwa unaowaongoza ni kuhamasisha uwajibikaji wa gharama nafuu. Kiongozi unapokubalika unakuwa umesaidia kujenga saikolojia za unaowaongoza na kwamba watafanya kazi kwa hiyari.
Ninawashukuru kwa mara nyengine kwa kunialika katika hafla hii adhimu na muhimu kwa nchi yetu na kweli najisikia faraja kuwa na Walimu Wakuu kwani name niliwahi kuwa mwalimu.
Nakutakieni hafla njema, yenye kila la kheri na Baraka. Aidha, hakikisheni kuwa umoja wenu huu unaendelea na unadumu ili warithi wenu wakukumbukeni milele.
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, nakutakieni mafanikio mema katika Mkutano wenu wa siku tatu na natamka rasmi kuwa Mkutano wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar umefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.