Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amepata mapokezi mengine makubwa kutoka kwa wafuasi wa Chadema, katika ziara yake ya siku ya pili wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Umati mkubwa wa wakaazi wa wilaya hiyo walijitokeza katika viwanja vya Kiganamo kumlaki kiongozi huyo, aliejipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania.
Kutoka Kigoma mjini hadi Kasulu ni umbali wa kilomita 95, lakini wananchi walitembea kwa miguu kumsikiliza kiongozi huyo huku msafara wake ukisindikizwa na pikipi zaidi ya 200.
Shughuli za biashara zilisimama kwa muda wakati msafara wa mapipiki ukipita, huku maduka mengi yakionekana kufungwa.
Akihutubia mkutano huo, Zitto alisema ataendelea kuwa mwanachama mtiifu wa Chadema hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa, lakini vyovyote iwavyo ataendelea kushirikiana na wananchi wa Kigoma.
Kuhusu mgogoro katika chama chake, alisisitiza kwamba mtu wa Kigoma kugombea uenyekiti wa Chadema sio uhaini, lakini mashtaka yote aliyoandaliwa na chama yalilenga kumlaumu kwa kutaka uenyekiti wa chama.
“Mimi sina chuki na mtu, lakini linapokuja suala la nchi na chama, mimi nachangia nchi kwanza chama baadae,” alisema.
Alisema ataendelea kutetea wananchi kwa kufanya kazi zake za Ubunge mpaka pale atakapokosa sifa za kufanya hivyo.
Wakati huohuo, habari zinasema baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA wamemuonya Zitto kwa kile wanachodai ukiukwaji wa waziwazi wa taratibu za chama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajumbe hao walishangazwa na kitendo cha Zitto kujiandalia ziara zenye mwelekeo hasi kwa chama hicho.
Kilichowashangaza wajumbe hao ni kitendo cha Mbunge huyo kufanya ziara jimbo la Kasulu bila kukitaarifu chama huku mashabiki wake wakiutumia mkutano huo kukashifu chama na viongozi wake.
Walisema kitendo kinachofanyika hakikubaliki na ni ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu za chama.