Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji waliojitolea kusaidia kuchangia sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Nusu Karne hapo Serena Hoteli Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katyika picha ya pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Nchini uturuki kwenye chakula cha usiku kilichofanyika Serena Hoteli Mjini Dar es salaam.( Picha na Hassan Issa OMPR)
Na Othman Ame OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwacha milango wazi kwa wawekezaji wa sekta tofauti kutoka Nchini Uturuki kuwekeza vitega uchumi vyao Visiwani Zanzibar kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Zanzibar za kuimarisha uchumi wake pamoja na kudumisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.
Fursa kadhaa za uwekezaji katika sekta ya Kilimo, Utalii na afya bado zipo kutokana na washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi kujengewa mazingira mazuri na Serikali ya miundo mbinu ya uwekezaji katika maeneo hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa chakula cha usiku kilichojumuisha wafanyabiashara wa sekta tofauti ndani na nje ya nchi waliojitolea kuchangia harakati za sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia nusu karne.
Balozi Seif aliwaeleza wafanyabiashara hayo aliojumuika nao pamoja katika ukumbi wa Serenna Hoteli Jijini Dar es salaam kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko katika jitihada za kunyanyua uchumi wake katika kubuni sekta mbali mbali ili kusaidia zao la Karafuu ambalo ndilo muhimili wa uchumi hivi sasa likisaidiwa na sekta ya Utalii.
Akizungumzia maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka hamsini ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamuwa kuzifanya sherehe za mwaka 2014 kuwa kubwa za aina yake kutokana na Mapinduzi hayo kufikisha Nusu karne.
Alisema uamuzi huo wa Serikali umekuja ili kuwaenzi waasisi wa mapinduzi hayo ambao walipigania haki ya kujikomboa kitendo ambacho kimeleta faraja na mabadiliko makubwa ya kiuchumi miongoni mwa wananchi wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewashukuru na kuwapongeza wafanyabiashara waliojitolea na kuweka ahadi ya kuchangia mambo mbali mbali kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo za Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif alisema michango ya wafanyabiashara hao pamoja na washirika wa maendeleo imeleta faraja na matumaini makubwa kwa Serikali pamoja na Wananchi wote hapa Nchini.
Mapema wafanyabiashara hao wakiwakilishwa na Mzee Bashir walieleza kwamba wataendelea kuyaeshimu Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo ndio yaliyozaa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Wafanyabiashara hao walisema wako tayari kuchangia kwa hali na mali kufanikisha sherehe hizo zinazotarajiwa kubwa na za aina yake mwaka ujao wa 2014.
Zaidi ya shilingi Milioni 65,000,000/- zimeahidiwa kutolewa na wafanyabiashara hao kwa ajili ya kuchangia shsrehe hizo za Kihistoria.