Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Nahodha: Sitavunjika moyo kwa yaliyonikuta

$
0
0
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha amesema licha ya kuvuliwa uwaziri ataendelea kuwa kiongozi wa kisiasa na kukitumikia chama chake na wananchi bila ya kuvunjika moyo.
 
Nahodha, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kuondolewa kwenye Baraza la Mawaziri na Rais Jakaya Kikwete kutokana na matatizo yaliyotokea katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Akihutubia wanachama wa CCM waliomlaki na kumsikiliza kwenye Ofisi ya chama hicho Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja jana, Nahodha alisema yaliyomtokea ni mambo ya kawaida katika medani za utumishi wa umma.
“Pamoja na hayo yaliyotokea, nitaendelea kulitumikia taifa, chama changu na wananchi kwa uaminifu, juhudi na uwezo wangu wote,” alisema Nahodha, ambaye pia ni Mwakilishi wa Mwanakerekwe.
Alisema amewajibika serikalini kutokana na matakwa ya wajibu katika utendaji wa pamoja na kusema kitendo hicho ni mfano wa ajali inayoweza kumkuta mtu yeyote katika safari ya maisha.

“Sina kinyongo wala muhali, yaliyotokea ni mambo ya kawaida katika medani za uongozi, wajibu na dhati yangu ni kuwa mtii kwa Serikali zote. Pia kuitumikia CCM na kushirikiana na wananchi wenzangu. Binadamu hawezi kujiepusha na mitihani, ”alisema Nahodha.
Alisema alikabidhiwa dhamana na viongozi wake ili kulitumikia taifa na kutimiza wajibu ipasavyo katika nyadhifa mbalimbali na yaliyomtokea ameyapokea kwa mikono miwili na hana kinyongo.
Mawaziri walioenguliwa pamoja na Nahodha ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Dk Mathayo David (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).
Mapinduzi ya Zanzibar
Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar, Nahodha alisema ni ufunguo uliofungua milango ya fursa kwa wananchi wanyonge waliokandamizwa na ukoloni huku akisifu uongozi kwa miaka minane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema kiongozi huyo licha ya kuongoza Mapinduzi ya Januari 12, 1964, aliifanyia mema Zanzibar na watu wake katika kuwaletea maendeleo na kwamba atakumbukwa na vizazi vyote hadi mwisho wa dunia.
 
“Kufanya Mapinduzi haikuwa kazi nyepesi. Waliofanya walikuwa ni majasiri na wazalendo. Juhudi zao ni matunda haya leo baada ya miaka 50 kupita nchi ikiwa katika utulivu na amani,” alisema Nahodha, ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kuanzia mwaka 2000 hadi 2010.
“Uongozi wa Mzee Karume ni mfano wa aina yake, mwaka 1964 hadi 1972 aliiletea mabadiliko makubwa Zanzibar. Alijenga viwanda, makazi bora, elimu bila malipo, barabara na kuimarisha huduma za jamii,” alisema Nahodha.
“Nasikia kuna watu hawataki kulisikia neno Mapinduzi, hao ni wapuuzi na wapuuzeni. Mapinduzi na Muungano ni uti wetu wa mgongo, Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Karume waliona mbali, tusibeze mitazamo yao kwa tamaa za madaraka,” alisema.
Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nahodha alisema angependa ubaki katika mfumo na Serikali mbili na kusema pamoja na uzuri wake, zipo changamoto na kasoro zinazohitaji kurekebishwa na kuwa na muungano wenye nguvu za kiuchumi.
 
Alisema kazi ya kurekebisha makosa ni nyepesi lakini wazo la kuvunja Muungano lina gharama kubwa kuliko inavyofikiriwa na baadhi ya watu wanaotaka uvunjike.
“Sina uwezo wa kuwachagulia watu kitu wanachokipenda na kukitamani. Imani yangu ni kwamba nje ya Muungano hatutabaki salama kama ilivyo sasa. Muungano wetu umekuwa kinga na nguzo kwa nchi zetu mbili na usalama na wake,” alisema Nahodha.
Aliitolea mfano Sudan Kusini ambayo ilitaka ipewe mamlaka yake kamili akisema hivi sasa imejikuta ikiwa katika machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kuibuka kwa mgawanyiko wa kijamii unaotishia mustakabali wa Taifa hilo.
“Itazameni Sudan Kusini, tusipokuwa waangalifu na makini yanaweza kutukuta. Angalia vita ya Somalia inaitesa Kenya na kutukosesha amani, tusikubali kugawanywa na viongozi ambao wanawaza madaraka.”
 
Chanzo : Mwananchi

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>