Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Hawawataki Wapemba, wanataka karafuu zao

$
0
0
Na Salim Said Salim
 
UPO usemi maarufu wa  kiswahili tokea dahari na enzi unaotumika sana Zanzibar usemao; “Baniani mbaya, kiatu chake dawa”.
 
Usemi huu ulitokana na hali iliyokuwapo hapo zamani ya watu wengi wa Visiwani kuwaangalia kwa ubaya na kutowaamini mabaniani (watu wa jamii ya Hindu kutoka India). Hawa mabaniani walikuwa maarufu kwa kushona viatu, hasa vya kiume.
Lakini pamoja na kumuoa baniani kuwa ni mbaya, bado watu wengi walikuwa hawaridhiki ilipofika mwezi mtukufu wa Ramadhani kama hawajaenda kwa baniani ili kumshonea  mtoto wake au hata mwenyewe viatu kwa ajili ya Sikukuu ya Idd el Fitr.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa baadhi ya baniani, licha kuonekana na jamii kuwa ni watu wabaya, walikuwa wakiwashonea watu viatu kwa mkopo, tena bila ya kuwatoza riba.
Baniani mmoja aliyekuwa akiitwa Surti katika Mji Mkongwe alikuwa na msemo maarufu alipokuwa akitoa mkopo kwa kusema; “Vaa buti leo, lipa pesa kesho”.
 
Hali hii ndio iliyozaa msemo huu wa “Baniani mbaya, kiatu chake dawa”. Ndiyo hali inayojitokeza waziwazi Zanzibar katika siasa zilizopitwa na wakati za wahafidhina na baadhi ya wastaafu wa vikosi vya ulinzi na usalama ambao wanaona fahari kupalilia mbegu za siasa za chuki, uhasama, ubaguzi na ufashisti.

Ukiutafakari mwenendo wa hawa wahafidhina na wastaafu ambao wanaonekana kuogopwa na serikali na ndiyo maana hawawajibishwi kisheria kwa kauli zao za uchochezi na ubaguzi, utaona waliowashikia bango zaidi ni watu wa Kisiwa cha Pemba.
Ukiangalia kwa undani utaona hapana lolote lile lililosababisha kujengeka kwa hizo chuki, isipokuwa wivu na uhasidi unaotokana na Wapemba kupata mafanikio makubwa ya kimaisha. Hii inatokana na ukweli kwamba Wapemba ni watu wa kujituma zaidi kuliko wenzao wa Kisiwa cha Unguja kadiri ya muono wangu.
Wakati kijana mwenye asili ya Kisiwa cha Pemba anaweza kufanya kazi ya sulubu kabla ya jua kuchomoza hadi linapozama huku akipumzika kwa muda mchache, na kuendelea tena na kazi nyingine kwa saa mbili ama tatu wakati wa usiku, vijana wengi wa Unguja huona wamefanya kazi sana kama wakitumia saa tatu au nne!
Hali hii inatokana na umwinyi, kupenda makubwa na maisha ya fahari, kunakoonekana zaidi miongoni mwa vijana wa Kisiwa cha Unguja kuliko wenzao wa Kisiwa cha Pemba.
Lakini wakati wahafidhina na wastaafu wakiimba nyimbo zao chafu za kuwataka Wapemba waliopo Unguja warudi kwao (ati Unguja na Pemba hazina historia ya watu wake kuwa wamoja), siwasikii kusema na hizi karafuu ambazo kila baaada ya siku chache huletwa kwa wingi kutoka Pemba kuja Unguja zibakie huko huko Pemba.
Kwa maana hiyo, hawa wanafiki wa kisiasa hawawataki Wapemba kwa sababu ya msimamo wao wa kisiasa wa kuwa wapinzani, lakini wanazipenda karafuu zinazotoka Pemba.
Taarifa ya serikali ya hivi karibuni imeeleza kuwa Shirika la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZSTC) hadi wiki iliyopita limeshanunua tani 1,500 za karafuu kisiwani Pemba kwa msimu huu, na zoezi hilo linaendelea kwa kasi nzuri.
Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Biashara wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema kazi ya uchumaji wa karafuu inaendelea vizuri Pemba na lengo ni kwa  ZSTC kununua zaidi ya tani 4,500 msimu huu.
Wakati Pemba imeshachuma na kuuza serikalini zaidi ya tani 1,500, Kisiwa cha Unguja ndiyo kwanza kinajikongoja kukaribia kuuza tani 300 na kikifikia tani 1,000 mwishoni mwa msimu itakuwa maajabu.
Kwa kawaida Pemba huzalisha zaidi ya robo tatu ya zao lote la karafuu la Zanzibar ambalo kwa miaka mingi limechangia zaidi ya asilimia 90 ya pato lake la fedha za kigeni. Mchango huo sasa umeshuka na kuwa kati ya asilimia 35 hadi 40.
Fedha za karafuu nje ya nchi ndizo zinaipa serikali kwa kiasi kikubwa ubavu wa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo Unguja na Pemba. Vile vile, fedha hizi ndizo zinazowalipa mishahara hao wastaafu na wahafidhina, pamoja na kiinua mgongo na posho wanayoipata kila mwezi.
Kinachonishangaza na ninawauliza wahafidhina na wastaafu, wakiwemo wale wanaosalisha  Ijumaa waumini wa dini ya Kiislamu, mbona siwasikii kuitaka serikali iziache hizi karafuu Pemba badala ya kuzileta Unguja? Ama hawakukosea waswahili waliposema “Baniani mbaya, kiatu chake dawa”?
 
Kwa hakika watu wa Pemba wanapaswa kupongezwa kwa kuonyesha uzalendo wa kuitikia wito wa serikali wa kuuza karafuu zao kwa ZSTC na kuacha kuzisafirisha nje kwa magendo ambayo yangeweza kuwapatia bei kubwa zaidi.
ZSTC imebahatika kununua tani 1,500 za karafuu kwa msimu mzima kutoka Pemba. Hii ilitokana na karafuu nyingi, zaidi ya nusu, kusafirishwa kwa magendo nje ya Zanzibar.
Lakini serikali nayo inafaa kupongezwa kwa kusikiliza kilio cha Wapemba cha kuomba unyonyaji waliokuwa wakitendewa kama haukuweza kuondoshwa basi angalu upunguzwe ili na wao wapumue.
Kwa muda mrefu Mpemba alipata sio zaidi ya asilimia 50 (upo wakati alilipwa asilimia 2.25) ya bei ya soko la dunia. Hivi sasa mkulima wa karafuu analipwa kati ya asilimia 78 na 82 ya bei ya soko la dunia ambayo hupanda na kushuka baada ya kila kipindi kifupi.
Kwa vyovyote vile, hatua ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais Ali Mohamed Shein, inafaa kupongezwa kwa kuonyesha kuwajali wakulima wa Pemba kwa kuongeza bei ya kuuza karafuu. Hali hii imewafurahisha Wapemba ambao kwa miaka mingi wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar, lakini hawatendewi haki kwa malipo ya karafuu.
Ni matarajio yangu uzalendo ulioonyeshwa na Wapemba kwa nchi yao unafaa uwe somo kwa wahafidhina ambao wamejenga chuki zisizokuwa na msingi, isipokuwa husuda tu kwa Wapemba.
Ni vyema wahafidhina sio tu wakaachana na kumkataa baniani na kupenda kiatu chake, lakini wakabadilika na kuanza kampeni ya kuwataka watu wa Unguja nao wachangie pakubwa zaidi uchumi wa nchi yao kama wanavyofanya ndugu zao wa Pemba.
Umoja na sio fitna za kibaguzi ndio utakaojenga Zanzibar na hili wajue sio wahafidhina tu, bali hata wale wenye ndoto ya kuwagawa hata watu wa Kisiwa cha Unguja kwa makabila au maeneo wanayotoka ya mjini na mashamba, kaskazini na kusini.
Wakati Wazanzibari wakisherehekea miaka 50 ya mapinduzi na kumalizika sherehe hizi zilizogharimu mabilioni ya shilingi na kuanza safari mpya ya kujitafutia maendeleo, ni vizuri kwa watu wote Visiwani, Unguja na Pemba, kuachana na siasa za chuki, uhasama na ubaguzi.
Ni umoja tu na maelewano, licha ya tofauti zao za kisiasa ndio utakaoweza kuwapatia maendeleo wao na vizazi vijavyo.
 
Chanzo : Tanzania Daima

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles