Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema mapato ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kwa mwezi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2023/2024 hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni moja mwaka 2024/2025.
Amesema ongezeko hilo limetokana na uboreshaji wa bandari zilizo katika Bahari na uwekezaji wa sekta binafsi katika kutoa baadhi ya huduma bandarini.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mapato yanayokusanywa kutokana na ushuru wa forodha yameongezeka kutoka shilingi trilioni 9.35 mwaka 2023/2024 hadi shilingi trillioni 9.86 kufikia Februari 2025.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 9, 2025) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Mtumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.
Pia, Waziri Mkuu amesema idadi ya makasha yanayohudumiwa yameongezeka na kufikia 686,515 katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Februari, 2025 ikilinganishwa na makasha 670,724 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ongezeko hilo lilichangiwa na uwekezaji uliofanyika katika gati 0 - 7 ambapo idadi ya makasha yaliyohudumiwa katika eneo hilo yaliongezeka kutoka 122,339 hadi 160,286 katika kipindi hicho.
Aidha, Waziri Mkuu amesema muda wa meli za makasha kusubiri nangani umeondolewa kabisa. Hivi sasa, meli hufunga gatini mara zinapowasili katika Bandari ya Dar es Salaam. “Hali hiyo imepunguza wastani wa muda wa meli zisizo za makasha kusubiri nangani kutoka siku 46 za awali hadi siku saba.”
Amesema kwa kuzingatia ushindani wa kibiashara uliopo katika ukanda wa Bahari ya Hindi, Tanzania imechukua hatua mahsusi ili kunufaika na fursa ya kijiografia ya kuwa lango kuu la kibiashara kwa nchi jirani.
“Mafanikio mengine yaliyopatikana katika Bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na kupungua kwa idadi ya meli zinazo subiria nangani kutoka meli 30 hadi tatu; muda wa meli kuhudumiwa umepungua kutoka siku nane hadi tatu kwa meli za makasha.”
Pia, Waziri Mkuu amesema muda wa kuhudumia meli za mafuta umepungua kutoka siku 10 hadi siku tatu, kuimarika kwa utoaji wa huduma hizo kumepunguza tozo ya meli kusubiri nangani na hivyo kuchangia kupunguza gharama za bidhaa kwa Watanzania.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2024 pato halisi la Taifa limekua kwa wastani wa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Amesema ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme; uimarishaji wa huduma za jamii; kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi; kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji; na kuimarika kwa sekta ya uchukuzi.
Amesema kuwa mwenendo wa viashiria vya uchumi na bajeti katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024/2025 umeendelea kuwa wa kuridhisha.
“Sekta zilizokuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji katika kipindi cha marejeo ni pamoja na shughuli za fedha na bima zilizokuwa na ukuaji wa asilimia 17.1, umeme asilimia 15.5 na habari na mawasiliano asilimia 12.4.”
(mwisho)