Kauthar Abdalla na Asya Hassan
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameijadili na kuipitisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa mwaka 2013/2014.
Akitoa majumuisho ya hoja zilizochangiwa na wajumbe mbali mbali wa Baraza hilo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, alisema ili kwenda sambamba na bajeti ya matumizi yaliyopangwa Wizara hiyo imeandaa sera ya elimu mjumuisho itakayozingatia wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuweka utofauti katika utungaji wa mitihani yao.
Waziri alisema ili kuondosha usumbufu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum Wizara imeona ipo haja ya kuandaa sera hiyo ili kuona wanafunzi wanatungiwa mitihani inayokwenda sambamba na mazingira waliyonayo.
Alifahamisha kuwa tatizo la posho kwa walimu wa elimu mjumuisho limeongezeka kutoka shilingi 5,000 hadi kufikia 30,000 kuanzia Julai mwaka huu ili kuwapa nguvu zaidi walimu hao, ambapo pia walimu wakuu na wasaidizi wao wataongezewa posho.
Alisema suala la mporomoko wa maadili kwa baadhi ya walimu na wananfunzi bado ni kubwa kutokana na kutofuata mwenendo na sheria za elimu jambo ambalo linapelekea kupunguza kasi ya kiwango cha elimu.
Akizungumzia suala la adabu mbadala katika skuli alisema suala hilo lipo kwa majaribio lakini linaonekana linakidhi haja ya kuwepo kwa adabu hiyo.
Alifahamisha kuwa kuendelezwa kwa matumizi ya bakora skuli kunajenga uadui kati ya walimu, wazazi pamoja na wanafunzi kwa kutotumiwa bakora ipasavyo kwani baadhi ya walimu huwapiga wanafunzi kwa chuki bila ya kosa la msingi na kupelekea madhara.
Pia alisema Wizara haina uwezo wa kutekeleza kazi zote za wananchi ikiwemo kukamilisha ujenzi wa majengo ya skuli yaliyoanzwa kujengwa na wananchi kutokana na ufinyu wa bajeti wanayoipata.
Akigusia suala la kufeli kwa wanafunzi Waziri huyo alisema ni suala mtambuka ambalo linachangiwa na mambo ikiwemo walimu, upungufu wa vifaa,maadili pamoja na mambo ya utandawazi ambao wanafunzi wengi hujishirikisha katika mitandao na kuangalia mambo ya nje ya elimu.
Alielezea kuwa kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana kumetokana na mitihani na sio upendeleo wala makusudi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Akitaja sababu nyengine ya kufeli kwa wanafunzi hao alisema ni kubadilishwa kwa utaratibu wa upangaji wa maksi bila ya kuwaandaa walimu kwani huwa hakuna kiwango sahihi cha maksi.
Sambamba na hayo Waziri alisema Wizara yake inatarajia kufanya kongamano la kitaifa litakaloshirikisha wadau mbali mbali ili kuweza kujadili matokeo ya kidato cha nne ili kudhibiti hali ya matokeo ya mwaka jana isitokee tena.
Nae Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Zahra Ali Hamadi alisema sera ya elimu ya wizara yake ina lengo la kujenga skuli za ghorofa ili kupunguza tatizo la uhaba wa nafasi kwa skuli za Zanzibar.
Naibu alisema suala la uvamizi wa maeneo ya skuli lina umuhimu mkubwa kudhibitiwa ambapo Serikali kupitia Wizara ya elimu ipo hatua za kuzipatia hatimilikiza majengo ya skuli ili kudhitibiti hali hiyo.
Akizungumzia tatizo la kuhamishwa kwa walimu kutoka skuli moja kwenda skuli nyengine alisema linategemea mahitaji ya skuli husika na sio suala la upendeleo kwa b aadhi ya walimu.
Akichangia Bajeti hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir alisema kuwa suala la ajira ni tatizo sugu ambalo inalikabili taasisi zote za serikali na sio kwa walimu pekee.
Alisema sekta zote za serikali zinakabiliwa na tatizo la ajira lakini linashindwa kufanyiwa kazi kutokana na ufinyu wa bajeti.
Waziri huyo alifahamisha kuwa ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo la ajira serikali ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kuanzisha ajira za nafasi mbalimbali katika sekta binafsi ili kuweza kupunguza tatizo hilo na kuboresha maisha ya wananchi.