Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Kificho achukua Fomu kuwania uenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba

$
0
0
Wakati Bunge la Katiba linaanza rasmi leo mjini Dodoma, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ameir Pandu Kificho, amechukua fomu kuwania uenyekiti wa muda wa Bunge hilo.

Kificho alichukua fomu hizo jana mchana baada ya mchakato wa kuchukua fomu hizo kuanza.

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dk. Thomas Kashililah, alithibitisha jana jioni kuwa Kificho amechukua fomu hizo akiwa mgombea wa kwanza kuzichukua huku wengine wakitarajiwa kuzichukua mapema leo kabla uchaguzi kufanyika mchana.

Wajumbe wa Bunge hilo leo watamchagua mwenyekiti wa muda atakayesimamia uandaaji na upitishaji wa kanuni na michakato mbalimbali, ikiwamo uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake wa kudumu wa Bunge hilo.
 

Mwenyekiti wa muda Bunge hilo na makamu wake, pamoja na mambo mengine, watakuwa na jukumu la kusimamia upitishaji wa kanuni na kusimamia uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu na makamu wake.

Dk. Kashililah alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.Alisema uchaguzi huo utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana.

Alisema mwenyekiti huyo atatakiwa kuwa na wadhamini 10 ambao ni wajumbe wa Bunge la Katiba.

 “Kikao cha kesho (leo) asubuhi hakitakuwa na mwenyekiti, kwa hiyo kitaongozwa na makatibu wa Bunge na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, baadaye sisi tutarajie jina la mtu akatakayekaa kwenye kiti kuongoza mchakato wa kumpata mwenyekiti wa muda,” alisema Dk. Kashililah.

“Sisi ni wasimamizi wa uchaguzi, hivyo tutaendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi…uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake tunasubiri kanuni zitakazopitishwa na wajumbe.”

“Ili zitungwe ni lazima wachaguliwe mwenyekiti na makamu wake wachaguliwe na wajumbe wenyewe…kesho (leo) makatibu tumepewa dhamana ya kuongoza kikao kwanza tu.”

Kesho na Alhamisi kutakuwa na kikao cha kazi ya kuandaa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum itakayofanyika nje ya Bunge na Ijumaa kutakuwa na kikao cha azimio la kuridhia Kanuni za Bunge na uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu na makamu wake.

Wote wataapa kiapo pamoja na wajumbe wa Bunge Maalumu Jumamosi.Jumapili hadi Jumatatu asubuhi na jioni yake ufunguzi rasmi.

Kuhusu kurusha matangazo ‘live’Dk. Kashililah alisema vituo vyote vya televisheni vinaruhusiwa kuwasilisha maombi ya kurusha matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja baada ya kukamilisha taratibu za kufanya hivyo.

CHENGE: MUDA BADO

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia nia yake ya kuwania uenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo kwa kuwa muda wa kuchukua fomu bado.

Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, ni miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo wanaotajwa kuwa wana nia ya kugombea nafasi hiyo.

Chenge aaambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na msimamo wake, jana kuhusiana na kugombea nafasi hiyo, alisema kuwa muda wa kuchukua fomu bado.

“Bado muda, niacheni kwanza nikajiandikishe (kujisajili), bado muda,” alisema Chenge.

KIFICHO: SIWANII  UENYEKITI WA KUDUMU

Kwa upande wake, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ameir Pandu Kificho, amesema hana nia ya kuwania uenyekiti wa kudumu wa Bunge la Katiba.

Kificho amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo. Hata hivyo, jana alipoulizwa na NIPASHE, mjini Dodoma alijibu kwa kifupi kuwa: ”Sina nia ya kugombea, nafasi hiyo, mimi nitakuwa mchangiaji, wenzangu watachukua nafasi.”

Mbali na Chenge, Kificho wajumbe wengine ambao wanatajwa kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda.

Imeandikwa na John Ngunge, Muhib Said na Salome Kitomari, Dodoma

CHANZO: NIPASHE

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>