Na kadama Malunde, Shinyanga
ASILIMIA 70 ya Watanzania wanaohukumiwa vifungo magerezani, wanafungwa kwa sababu ya kutojua sheria na kutopata msaada wa kisheria.
Hali hiyo imebainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo viongozi wa asasi zinazojishughulisha na utoaji wa huduma za kisheria mkoani Shinyanga yaliyoendeshwa na Mtandao wa watoa huduma wa msaada wa kisheria nchini (TANLAP).
Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo,Edna Bakebwa, ambaye ni mwanasheria wa kutoka TANLAP, alisema utafiti uliofanywa hivi karibuni umebaini asilimia 70 ya watu waliomo magerezani walitiwa hatiani kutokana na kutozijua vyema sheria za nchi.
Alisema kutokana na kutojua haki huwafanya kushindwa kujitetea vizuri na hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuielimisha jamii kujua haki zao.
Alisema watoa huduma za kisheria wana fursa ya kuwatembelea wafungwa waliomo magerezani na kuelimishwa juu ya haki zao za msingi kwa mujibu wa katiba ya nchi na kwamba kwa wale wanaofikishwa katika vituo vya polisi wanayo haki ya kutoa maelezo yao mbele ya mtu au wakili wanayemtaka.
Katika hatua nyingine alisema si tabia nzuri ya watoa huduma za msaada wa kisheria kukaa bila ya kuielimisha jamii juu ya haki zao za msingi na kusubiri mpaka pale wanapopatwa na matatizo ndipo hujitokeza kwenda mahakamani kuwapatia msaada wa kisheria.
“Katika utafiti uliofanywa mwaka 2011/2012 tulibaini asilimia 70 ya watu waliomo magerezani walifungwa kutokana na kutozijua sheria za nchi na hata haki zao za msingi kwa mujibu wa katiba, sasa hili ni tatizo ambalo nyinyi kama watoa huduma za msaada wa kisheria mnapaswa kulifanyia kazi,” alisema.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wamewaomba wajumbe wa bunge maalumu la katiba kuhakikisha wanajadili rasimu ya pili bila ya kutanguliza maslahi ya vyama vyao