Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) leo kitazindua ripoti ya utafiti wa unyanyasaji wa kijinsia uliofanyika Disemba 2013 katika wilaya 20 za Tanzania Bara na Zanzibar .Uzinduzi huo utafanyika ofisi za TAMWA Sinza Mori Dar es Salaaam.
Uzinduzi huo ni kutokana na utafiti uliofanyika baada ya mafunzo kutolewa kwa waandishi wa habari juu ya habari za uchunguzi dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA).
Ripotii hiyo inaonyesha hali halisi ya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii pamoja na mambo yanayokwamisha juhudi za vyombo vinavyotetea haki za wanawake na watoto nchini.
Utafiti huo ulifanywa kwa kushirikiana na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya Zanzibar Leo, Nipashe, The Guardian, The Citizen, Mwananchi, Daily News, Majira na Kituo cha Televisheni cha ITV.
Taarifa ya TAMWA ilisema katika utafiti huo waandishi wa habari waliweza kuwahoji wanajamii mbalimbali kuanzia ngazi za familia na kupata ukweli wa hali halisi ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo, ukeketaji, ubakaji, mauaji ya vikongwe, mimba katika umri mdogo na watoto wa kike kulazimishwa kuolewa.
Wilaya ziliyofanyiwa utafiti ni Kahama, Tarime, Sengerema, Newala, Mbulu, Singida Vijijini, Bariadi, Busega, Nkasi, Dodoma, Babati, Chunya na Bunda.
Kwa upande wa Zanzibar utafiti ulifanywa katika wilaya sita za mikoa ya mjini magharibi, kusini Pemba, kaskazini Pemba, Unguja kusini na kaskazini Unguja.