Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Mapinduzi kimewapa onyo kali makada wake sita wanaotuhumiwa kupiga kampeni za urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema baada ya makada hao kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazowakabili,ilithibitika baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na hivyo kupendekeza adhabu.
Alisema mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.
Makada hao ni waliokuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye na Edward Lowasa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge William Ngeleja.
Nape alisema kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa mawili ikiwemo kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM.
Kosa jengine ni kuthibtika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Alisema kosa hili nalo ni kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010.
Alisema kamati kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo chama kitawachukulia hatua kali zaidi.
Alisema tafsiri ya adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa kanuni za CCM, mtu aliyepewa adhabu ya onyo kali atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.
Aidha alisema kamati kuu imeitaka pia kamati ndogo ya udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja kanuni za chama.
Pia alisema kamati kuu imewaonya vikali viongozi na watendaji wa chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanaowania urais yanayovunja na kukiuka maadili ya chama.