Na Amina Omari, Tanga.
TABIA ya benki kuficha siri za wateja, zinachangia utoroshaji wa mabilioni ya fedha kutoka bara la Afrika na kuwaacha Waafrika wakibaki masikini.
Ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali imeshauriwa kupitia upya na kuzifanyia marekebisho sheria kinzani zinazotoa mwanya kwa vigogo wasio wazalendo kutorosha nje fedha.
Ushauri huo ulitolewa jana na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Tanga, Edson Makalo, wakati akifungua mafunzo ya siku 14 ya wakaguzi wa fedha na wakaguzi wa ndani wa hesabu kutoka taasisi za serikali.
Alisema mfumo uliopo sasa wa sheria ya benki kuficha siri za wateja umekuwa ukiathiri kwa kiasi kikubwa kazi za uchunguzi wa fedha zinazotoroshwa na baadhi ya waliopewa dhamana ya kuzitunza fedha za umma.
"Ili kupambana na rushwa kubwa za utoroshaji wa fedha nje ya nchi kuna kila haja ya kuzipitia upya na kuzifanyia marekebisho sheria kinzani hasa za usiri wa mabenki,"alisema.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chama cha Wakaguzi wa masuala yanayohusu udanganyifu wa fedha (ACFE) kanda ya Tanzania .
Katibu Matendaji wa chama hicho, Andendekisye Mwakabalula, alisema yatawezesha washiriki kupata mbinu za kisasa kwa kuwa wao ndio jicho la serikali.
"Washiriki hawa ni wakaguzi wa hesabu za ndani kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali nchini zikiwamo halmashauri za wilaya hivyo kupitia mafunzo haya tunaamini watakapomaliza watakuwa na mbinu mpya,"alisema.