Na Abdi Suleiman, PEMBA
WANAKAMATI ya Maendeleo shehia ya Mbuzini, jimbo la Ziwani wilaya ya Chake Chake Pemba, wametakiwa kushrikiana na wadau wote wa maendeleo pamoja na viongozi wa majimbo, ili kuyatatua matatizo yanayowakabili.
Wito huo umetolewa na mkufunzi Ali Abdalla Mbarouk, wakati akijadili jinsi ya kuandaa mpango mkakati kwa wanakamati ya maendeleo ya shehia hiyo katika skuli ya Mbuzini.
Alisema wakati umefika kwa wanakamati kuwa kitu kimoja katika kutafuta maendeleo ya shehia yao .
Alisema shehia ya Mbuzini inakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo suala la elimu na maji ambayo yameonekana kuwa ndio kikwazo kikubwa.
Changamoto nyenginei ni upungufu wa madarasa ya kusomea, upungufu wa walimu wa sayansi, vitendea kazi maskulini na uharibifu wa mazingira.
Hata hivyo, alisema muda umeshapita wa kutegemea serikali kwa kila kitu, hivyo wanakamati hawana budi kuwa mstari wa mbele kutekeleza na kuondoa kero zinazowakabili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo, Fatma Mohame Omar, alisema lengo la kuanzisha kamati ni kuitikia sera ya nchi inayotaka kila shehia kuwa na kamati ya maendeleo.
Alisema lengo ni kuhamasisha wanajami katika kuibua kero zao, pamoja na kuziondosha kezo zote zinazowakabili kwa pamoja.
Mafunzo hayo ya siku tano yamefadhiliwa na Foundation for Civil Society.