Na Kija Elias, MOSHI
MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Rashushi Shembusho, mkazi wa Pasu Matindigani, manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ametapeliwa shilingi milioni 5.4, katika hoteli ya Fresh Coach na watu wasiofahamika.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 3:00 asubuhi, wakati mwanamke huyo alipokutana na watu hao katika hoteli hiyo.
Katika mpango huo mwanamke huyo alikuwa atoe shilingi milioni 5 huku yeye akitegemea kupata dola za Marekani 6,172, sawa na shilingi milioni 10.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mfanyakazi wa hoteli hiyo, Alhadji Juma, alisema mwanamke huyo, alifika hotelini akiwa pekee na kuagiza juisi ya matunda lakini wakati anampelekea alikuja mwanamke mwengine akiwa amejitanda ushungi akakaa nae meza moja.
Alisema baadae alimuona mwanamke aliyejitanda shungi akitoa fedha kwenye pochi lake, fedha ambazo zilifanana na dola, zikiwa katika mafungu mawili.
Alisema muda mfupi baadaye mwanamke huyo aliondoka na kurejea huku akiwa amebeba pochi ambalo hakufahamu kilichokuwemo ndani.
Alisema baada ya kurejea hotelini, wanawake hao waliendelea na mazungumzo lakini muda mfupi alitokea kijana mmoja ambaye aliungana nao kabla ya kuondoka kwa mwendo wa haraka pamoja na yule mwanamke aliyejitanda shungi.
Aidha mhudumu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la God Mbise, alisema baada ya mwanamke huyo kupiga mayowe, walimfuata kwa lengo la kujua tatizo na kuwaambia ametapeliwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya kusaidiwa na wasamaria wema kutoa taarifa polisi, alisema alikuwa ametokea benki ya uchumi, iliyoko mjini Moshi kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 4.9 na kwamba kabla, ndani ya pochi yake kulikuwa na shilingi 500,000.
Alisema fedha hizo alizitoa kwa lengo la kumtumia mwanaye aliyeko Dar es Salaam kwa ajili ya kununua gari na wakati anatoka benki, alikutana na watu wawili, mwanamme na mwanamke ambaye alikuwa amejitanda shungi.
Alisema mwanamke alimuomba amuoneshe sehemu ya kubadilishia fedha kwani yeye ni mgeni (muarabu) kwa ahadi ya kumpa dola moja kama ahsante.
Alisema baada ya kupewa dola moja, alimpeleka duka la kubadilishia fedha ambalo liko jirani na ofisi za shirika la posta tawi la Moshi, kubadilisha fedha na baada ya kumaliza alimtaka waende mahali wakapate kinywaji.
Alisema walienda moja kwa moja hoteli ya Fresh Coach, wakiwa wote watatu na walipofika pale yule mwanamme alitoka na kuwaacha wakiwa wamekaa hotelini wakisubiri kuhudumiwa.
"Wakati wahudumu wamekuja kutusikiliza, yule dada, aliniomba nikamuite yule kaka ili aje apate kinywaji, lakini nilipokwenda kumfuata yule kijana sikumkuta na niliporudi nilishangaa kukuta yule mwanamke ameondoka pamoja na pochi langu lililokuwa na milioni 5.4 pamoja na kadi ya benki, simu na vitambulisho vyangu," alisema.
Juhudi za kumtafuta Kamanda wa polisi kuzungumzia tukio hilo zilizshindikana.
Kumekuwa na wimbi la utapeli katika siku za hivi karibuni katika maeneo ya benki ya CRDB, Malindi, NMB, benki ya posta na kituo kikuu cha mabasi Moshi.