STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 25 Februari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema uhusiano kati Tanzania na Zambia umekuwa bora wakati wote kutokana na misingi imara ya iliyowekwa na waasisi wa nchi hizo na ukaribu wa wananchi wa nchi mbili hizo.
Amesema Tanzania na Zambia zina mambo mengi yanayowaunganisha na kuziweka karibu na ndio maana wakati wote Serikali za nchi hizo zimekuwa zikifanya jitihada za kuendeleza na kuimarisha uhusiano huo.
Dk. Shein alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Zambia nchini Tanzania Bibi Judith Kangoma Kapijimpanga ambaye alifika Ikulu kujitambulisha.
“Kuna mambo mengi yanayotuunganisha na ni wakati sasa kuangalia maeneo zaidi ya kushirikiana ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano wetu”alisema Dk. Shein.
Alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na Zambia zinaweza kushirikiana katika masuala mengi kama vile utalii, kilimo hususan katika utafiti kwa kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar-ZARI na mafunzo kupitia Chuo Kikuu cha Zanzibar –SUZA.
Alibainisha kuwa angependa kuona kunakuwepo na ushirikiano wa kitaaluma kati ya ZARI na SUZA kwa upande mmoja na taasisi kama hizo nchini Zambia kwa upande wa pili ili kubadilishana uzoefu kwa njia ya kutembeleana walimu na wanafunzi wa taasisi na vyuo hivyo.
Kwa upande wake Balozi wa Zambia nchini Tanzania Bibi Judith Kangoma Kapijimpanga alisema ni dhamira ya Rais wa Zambia na wananchi wa nchi hiyo kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake wa kisiasa na kiuchumi na Tanzania.
“Hili si suala lililokuja kwa bahati mbaya bali linatokana na dhamira ya kweli waliokuwa nayo waasisi wa nchi zetu na viongozi wetu wa sasa” alisema Balozi Kapijimpanga.
Balozi huyo alimueleza Mhe Rais kuwa nchi yake inajivunia uhusiano wake na Tanzania ambapo mbali ya kuwa nchi hizo zimeweza kuweka historia ya kuanzisha reli ya pamoja TAZARA lakini pia zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali ikiwa ni kielelezo cha ushirikiano thabiti kati ya Serikali na watu wa nchi mbili hizo.
Amewasifu viongozi wa Tanzania kwa uongozi wao makini ambao umewezesha Tanzania kuendelea kuwa nchi ya mfano wa amani katika bara la Afrika.
Akijibu maelezo ya Mhe Rais kuhusu ushirikiano katika masuala ya kilimo na utafiti Balozi Kapijimpanga alisema nchini kwake kiko kituo cha utafiti cha kilimo cha Mount Makulu (Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zambia -ZARI) ambacho kimeweza kupiga hatua kubwa katika nyanja nyingi ikiwemo kuweza kutoa mbegu bora za muhogo ambazo haziwezi kushambulia na maradhi na kuzalisha mbu ambao wanaweza kudhibiti mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria.
Aliahidi kuwasilisha ujumbe huo kwa mamlaka husika nchinimkwake ili hatua za ushirikiano ziweze kuchukuliwa .
Balozi huyo amepokea kwa furaha wito wa Mhe Rais wa kubadilishana uzoefu katika masuala ya afya ikiwemo katika ngazi ufundishaji na utafiti na kueleza kuwa Zanzibar ineweza pia kufaidika na uzoefu wa nzchi yake katika usafhsjai na usanfu vito.
Balozi Kapijimpanga alieleza kuwa amefurahi kuona wanafunzi kutoka nchini wanapata fursa ya kuchukua masomo ya chuo kikuu hapa zanzobar ambapo wanasaidia kupata taaluma ambazo vyuo nchini Zambia havitoi masomo hayo.
“Wako hapa vijana kutoka Zambia wanachukua masomo ya sheria ya kislamu masomo ambayo hayafundishwi nchini kwetu hivyo ni ushirikiano mzuri unaosaidia nchi yetu kupata taaluma hiyo kutoka kwa ndugu zetu”alieleza Balozi huyo.
Wakati huo huo Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe Soud Ali Mohamed amesema uhusiano kati ya nchi yake Zanzibar ni wa kindugu na wa kihistoria na ndio maana kila mara Serikali na wananchi wa Oman wana nia na azma ya kukuza ushirikiano wake na Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Balozi Soud alisema hayo jana Ikulu wakati alipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambapo Balozi huyo alikwenda kujitambulisha.
Balozi Soud alibainisha kuwa jukumu lake kama Balozi wakati wote akiwa nchini ni kuhimiza na kukuza ushirikiano huo na kueleza kuwa matumaini yake ni kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi na wananchi wa Zanzibar katika kutimiza wajibu wake huo.
Naye Mhe Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimueleza Balozi Soud kuwa ni sahihi kuwa Zanzibar na Oman ni ndugu hivyo wana kila sababu ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano kati yao kwa faida ya nchi hizo na wananchi wake.
Dk. Shein alimhakikishia Balozi Soud kuwa Serikali na wananchi wa Zanzibar watampa ushirikiano kadri inavyowezekana kama ambavyo walifanya kwa watangulizi wake ili nae aweze kufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822