Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Waraka halali wa Muungano utumike Bunge la Katiba

$
0
0
Na Salim Said Salim
 
WASWAHILI wana msemo maarufu unaoeleza kuwa mambo kangaja huenda yakaja. Sasa wakati waheshimiwa wetu wa Bunge Maalumu la Katiba, baada ya baadhi yao kutaka waongezwe posho ili watuwakilishe vizuri katika kuitafutia nchi yetu Katiba mpya wanatarajiwa kuanza kazi iliyowapeleka Dodoma wakati wowote kuanzia sasa.
Kama wataongezewa posho nawapa hongera kwa kudai ‘haki’ yao na kama watakosa nawapa pole kwa ‘kudhulumiwa’.
 
Tukumbuke kuwa miaka michache tu iliyopita kuzungumzia kuwepo kwa Jamhuri ya Tanganyika (aulizwe Mtikila kwa yaliyomkuta na kundi  la G55 lilivyofungwa mdomo) na  kutaka mfumo wa serikali tatu wa Muungano ilikuwa ni dhambi kubwa nchini kwetu.
Baadhi ya wale waliothubutu kutoa kauli hizo au kuonyesha ishara ya kutaka hivyo walipambana na joto ya jiwe na hata baadhi yao kuambiwa kuwa si raia wa nchi hii. Yale yalikuwa mambo ya unyanyasaji wa hali ya juu (nawaonea imani waliobuni uchafu ule).
Visa hivi vilipokuwa vinaendelea marehemu rafiki yangu na mwana habari maarufu aliyeiaga dunia miaka minne iliyopita, Ali Nabwa, alikuwa akisema wakati ule kuwa kilichohitajika ni subira na ipo siku itakuwa kweli.

Nilipomweleza hatari ya kusubiri sana kwa mbichi kuwa mbivu huenda kukomalia kula iliyooza, aliniambia hao wanaokawilisha mageuzi ndio wataaokuja kula mzoga. Kweli sasa tunayaona.
Sasa ile siku itakuwa kweli aliyoizungumzia marehemu Nabwa imefika na ule msemo wa Waswahili wa mambo kangaja huenda yakaja umethibitisha usahihi wake.
Licha ya kuwepo kundi linalojipapatua kama kuku anayekata roho ili kutaka kuirudisha nchi inakotoka, kama vile hapakuwepo haja ya kukusanya maoni ya wananchi kwa vile wao ndio waamuzi wa nchi hii ielekee wapi, sasa ni wazi kuwa ile siku itakuwa kweli ndiyo hiyo inapiga hodi.
Shughuli za kuipitia rasimu ya pili ya Katiba ina mambo mengi na muhimu, kama kupunguza madaraka makubwa aliyokuwa nayo rais, uhuru wa kweli wa vyombo vya habari na mengi mengine ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu kuweza kujenga mfumo wa demokrasia ya kweli.
Lakini linalotawala mjadala wa wazi na kimya kimya, ukiachilia kilio cha wajumbe wa Katiba kutaka walipwe kama watoto wa kifalme badala ya watumishi wa umma, ni hili la Muungano wa serikali tatu.
Umma umetaka hivyo, lakini kina Ibni Kinana na Ibni Khuzaymat na Ibni Ilyas ambao wanaona nchi hii ni yao na wengine ni wapangaji bado hawataki kuridhia kinachotakiwa na wengi. Masikini roho zao kwa kutaka kumiliki kitu ambacho si chao peke yao.
Hapana ubishi kuwa inavyoonekana suala la mfumo wa Muungano ni moja kati ya mambo ambayo huenda yakatawala mjadala na kuchukua muda mrefu wa majadiliano na marekebisho ya hapa na pale. 
Lakini ninafikiri ingelikuwa vema kabla ya kulijadili suala hilo ni kwa wajumbe kuiona hati halisi ya mkataba uliounda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26, Aprili, mwaka 1964 na baadaye kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa muda mrefu pamekuwepo na shauku kubwa ya kuuona huu mkataba halisi, lakini kilichokuwa kinatolewa na baadhi ya viongozi wanaotaka kuendeleza mazoea ya kila wanachosema wao kiaminiwe tumeambiwa mkataba halisi upo.
Viongozi hawa hutueleza wana nia njema na nchi hii, lakini wao hawataki kukubali kuwa na wananchi wanayo nia njema na nchi yao.
Pamekuwepo na kauli nyingi zinazotofautiana juu ya kuwepo kwa karatasi halisi yenye sahihi za viongozi walioingia mkataba huu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheih Abeid Amani Karume.
Mapema mwaka jana tulimsikia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisema ile hati inayosakwa kwa udi na uvumbi na kusemekana haionekani ipo ndani ya meza moja katika jumba la Ikuku, Zanzibar.
Dk.Shein alishangaa kuona baadhi ya watu wanataka kujua ilipo hati ya Muungano, lakini hawajafanya juhudi za kuitafuta na kueleza kuwa nakala yake nyingine ipo makao makuu ya
Umoja wa Mataifa, New York.
Kwa maana hiyo wale waliojidai kufanya juhudi kubwa za kuipata walikuwa hawasemi kweli juu ya suala hili.
Kinachotatanisha na kukanganya jamii ni kuwa kumbukumbu zinaonyesha marais wastaafu, komandoo Salmin Amour Juma (awamu ya tano) na Dk. Amani Abeid Karume (awamu ya sita) wamenukuliwa wakisema, na hawakukanusha habari hizo zilipotoka kwenye magazeti, kuwa hawajawahi kuiona nakala hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Zanzibar baada ya Mapinduzi, marehemu Wolfango Dourado, aliwahi kusema hakuwahi kuiona hati hiyo na alikuwa na uhakika haikuwepo ofisini kwake.
Mwanasheria Mkuu mwingine, Idi Pandu Hassan, naye alinukuliwa kusema hajui lolote juu ya hati hiyo. Si hayo tu, Mahakama Kuu ya Zanzibar pia iliwahi kutoa tamko katika kesi iliyofunguliwa mahakamani kuwa haikuwa na taarifa ya wapi hati hiyo ipo.
Kama hiyo haitoshi, pia palikuwepo na kauli nyingine ya kutatanisha iliyotolewa katika Bunge mjini Dodoma na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Frederick Sumaye.
Bwana mkubwa huyu alisema (angalia kumbukumbu za Bunge na kama si kweli akanushe hakutoa kauli hiyo) kuwa hati ipo na aliahidi kuiwasilisha bungeni.
Lakini mpaka alipotoa mguu wake Bungeni kama mbunge na waziri mkuu, Sumaye hakuiwasilisha Bungeni hiyo hati na siku hizi haizungumzii kama vile hakuwapa Watanzania ahadi ambayo hajaitekeleza.
Sasa Bunge la Katiba linakutana na huu naona ndio wakati mzuri wa kuiwasilisha hati hii ili wajumbe waelewe wapi pa kuanzia.
Hati hii halisi ya mkataba wa Muungano ni muhimu na si filamu za picha ya Nyerere na Karume kuchanganya udongo wa nchi hizi mbili, Zanzibar na Tanganyia.
Watu hawa wawili walichanganya udongo na ukweli ni kuwa hivi sasa watu wengi wa pande hizi mbili wamechanganya damu katika miaka 50 ya Muungano wao.
Hata hivyo, bado ni muhimu kwao wao kujua walipotoka ili wafahamu hapa walipo na kupanga waeleekee wapi.
Kuuzungumzia Muungano bila ya kuwepo hati halisi itakuwa ni sawa na kuzunguka mbuyu na kutojua ni nani yupo mbele na nani yupo nyuma.
Tumesikia kauli nyingi juu ya mambo gani hasa yalikubaliwa kuwa ya Muungano na yapi si ya Muungano na jawabu hasa na la uhakika litapatikana katika waraka huu.
Suala linaloulizwa na wengi ni: Hii hati ipo wapi na kwa nini haiwekwi hadharani na hasa wakati huu wa mambo hadharani.
Kama hati imepotea kwa njia ambayo walioipoteza wanaijua na ni vema kwa serikali ikatoa tamko rasmi na wale wote ambao walisema ipo basi wawe na uungwana wa kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwadanganya.
Inawezekana utashi wa kisiasa ndio uliowapelekea kutoa kauli za kuwepo hati hii na kutupa maelezo ambayo bado mpaka leo hatujaona ukweli wake. Yote tisa, lililo muhimu ni kwa wajumbe wetu wa Baraza la Katiba kujadili rasimu ya pili kwa ustaarabu, heshima na ajabu na pasiwepo kulazimishana kukubali hoja au vitisho.
Zama za kutunishiana misuli zimepitwa na wakati na wanaojaribu watajikuta wanaadhirika na hawana pa kujificha.
Jingine muhimu ni kuelewa kuwa rasimu ya pili ya Katiba haikutoka moyoni mwa kiongozi wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba na wenzake, bali kwenye nyoyo za Watanzania.
Kwenda kinyume na matakwa na matarajio ya Watanzania itakuwa ndio usaliti mkubwa kuwahi kushuhudia katika historia ya nchi hii. Kama tumekuwa waongo na kulazimisha mambo kwa siku nyingi sasa tubadilike na kuwa wakweli na kuridhia linalotakiwa na wengi.
Wajumbe wote wa Bunge la Katiba lazima waelewe kuwa yale mambo kangaja huenda yakawa yamekuja na kwamba ile siku itakuwa kweli sasa imefika.
Tuifanye kazi ya kutengeneza Katiba mpya kwa heshima na adabu, kuaminiana na kuelewana na si kudanganyana na kutishana.
 Kila la heri Bunge Maalumu la Katiba, kuongezwa au kutoongezwa posho kusiwarudishe nyuma kuitumikia nchi hii kwa uadilifu. Historia ndiyo itayowahukumu.
 
Chanzo - Tanzania Daima

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>