Na Kauthar Abdalla
MTU mmoja amefariki dunia baada ya kupigwa rungu la kichwa kutokana na ugomvi wa familia.
Marehemu alipigwa rungu wakati alipokwenda kumpeleka rafiki yake nyumbani kwa dada yake kusuluhisha ugomvi ambao ulikuwepo uliohusisha mambo ya familia.
Tukio hilo lilitokea Nyarugusu wilaya ya magharibi Unguja.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo MKuu wa Operesheni ya Polisi Mkoa Kusini Unguja, Hamad Said Masoud, alisema kifo cha marehemu kilitokea Februari 22 mwaka wakati akipatiwa matibabu hospitali ya Mnazimmoja.
Alimtaja marehemu kuwa ni Mussa Haji Suleiman (20) mkaazi wa Mtopepo.
Alimtaja mtuhumiwa aliyesababisha mauaji hayo kuwa ni Malik Mohammed Ali (30) mkaazi wa Tomondo mjini Unguja ambae anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji.
Katika tukio jengine, mtu mmoja ameokotwa akiwa amefariki dunia karibu na kisima katika kijiji cha Cheju .
Alisema marehemu alifariki baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
Alisema marehemu aliyetambuliwa kwa jina la Kombo Khamis Makame mkaazi wa Muembemakumbi, alikutwa akiwa na majeraha mikononi na mguu wa kulia.