Na Kadama Malunde, Shinyanga.
BUNDI anaendelea kulia ndani ya chama cha CHADEMA baada ya Madiwani wawili wa chama hicho katika manispaa ya Shinyanga kutangaza kujiuzulu kwa madai kuwa uongozi ngazi ya taifa umeendelea kusikiliza majungu, kuwadhalilisha baadhi ya viongozi pamoja na kuwaita wasaliti.
Madiwani waliojiuzulu ni diwani wa kata ya Ngokolo, Sebastian Peter na Zacharia Mfuko kutoka kata ya Masekelo huku wakieleza kuwa wameamua kuchukua uamuzi huo kama ishara ya kuwajibika kwa niaba ya makosa yaliyofanywa na viongozi wa chama hicho kitaifa.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Naibu Meya wa manispaa hiyo, walisema wamekabidhi barua za kung’atuka kwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, ambae walidai ndie mwajiri wao.
Diwani wa kata ya Ngokolo, Sebastian Peter alitaja sababu tatu zilizopelekea kukuchua uamuzi huo.
“Ndugu waandishi wa habari sababu ya kwanza inatokana na kikundi cha Red brigade mwezi Novemba 2013 kuandika barua kwa Katibu Mkuu ambayo ililenga kuwadhalilisha viongozi wetu wa mkoa akiwemo Katibu wa mkoa, Nyangaki Shilungushela na Katibu wa wilaya, Siri Yasin kuwa wamehongwa kiasi cha shilingi milioni 90, tuhuma ambazo ni uongo,”alisema.
Alisema sababu ya pili ni Mwenyekiti wa taifa Freeman Mbowe, kuahihdi chama kitamaliza kujenga nyumba ya marehemu Philip Shelembi aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Shinyanga mjini, ahadi ambazo ameshindwa kuzisimamia.
Aidha alisema sababu ya tatu Mbowe amekuwa na tabia ya kuwaita baadhi ya wanachama wasaliti na wahaini, kauli ambazo hazipaswi kuzungumzwa na kiongozi wa juu wa chama.
“Chama hiki tumekijenga kwa siku nyingi, mimi ni miongoni mwa wanachama watakaokuwa wa mwisho kuamini kama kweli Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na wengine kuwa ni wasaliti wa chama,” alisema.
Kwa upande wake, diwani wa kata ya Masekelo, Zacharia Mfuko aliungana na diwani wa Ngokolo kuchukua maamuzi magumu na na kuongeza kuwa chama hicho kimekuwa kikifanya mambo kwa ubabaishaji.
“Katika kata yangu kulikuwa na sakata la Mweyekiti wa mtaa kukigawa kiwanja cha mwananchi wakati kuna kamati ya ugawaji, nilipokieleza chama walidai kulishughulikia lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea na uongozi wa chama umekaa kimya,” alisema.
Hata hivyo, madiwani hao walisema pamoja na kujivua nyadhifa zao za udiwani bado wataendelea kuwa wanachama wa Chadema kwani hawajawahi kuitwa kwenye kikao kuhojiwa kwa lolote na kwamba kwa muda wote waliokuwa madiwani na hawakuwa na mpango wa kujiunga na chama chengine.
Akizungumzia kuhusu maamuzi hayo, Katibu wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Nyangaki Shilungushela, alisema chama kimepata pigo kubwa lakini kitajipanga kikamilifu ili kurudisha kata hizo mikononi mwake.
Manispaa ya Shinyanga ilikuwa na madiwani wa CHADEMA wanane na sasa wamebaki sita huku Chama cha Mapinduzi kikiendelea kuwa na madiwani 17.