Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM
WAANDISHI wa habari 101 wameteuliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT) 2013 ambapo kilele chake kinatarajiwa kuwa Machi 14 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, alisema idadi ya wateule imeongezeka ambapo ni sawa na asilimia 24.6 ikilinganishwa na mwaka jana.
Alisema kwa mwaka huu idadi ya waandishi wa habari wanawake walioteuliwa imeongezeka na kufikia 18 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambao walikuwa 11 kwenye kinyang’anyiro hicho, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 63.6.
Alisema waandishi wa magazeti wako 46, radio 39 na televisheni 16.
“Wakati wateule kwenye magazeti wameongezeka kwa wateule watano ikilinganishwa na mwaka jana ambapo walikuwepo wateule 41, kwenye radio wameongezeka hadi kufikia 39 ikilinganishwa na 21 wa mwaka uliopita,” alisema.
Aidha alisema kwa upande wa televisheni idadi ya wateule imepungua kutoka 19 mwaka hadi kufikia 16.
Wakati mashindano hayo yalipoanza kulikuwa na makundi tisa ya kushindaniwa ambapo mwaka uliofuata yaliongezeka kufikia 16 na mwaka 2011 yalifika makundi 19.
Alisema jopo la majaji lilianza kupitia kazi za waandishi tangu Februari 10 na kumaliza kazi Februari 16 chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa majaji, Gervas Moshiro.
Sambasamba na EJAT jopo la wataalam wa tunzo za maisha ya mafanikio katika uandishi (LAJA) wamewasilisha pia majina ya wateule ambao watatangazwa katika tamasha hilo .
Aliwataja baadhi ya wateule hao kuwa ni Grace Kiondo, Rahma Ally, Husna Mohamed, Mwantanga Ame kutoka Zanzibar na Sam Mahela ITV na Gervas Hubile TBC kutoka Dar es Salaam .
Katika tamasha hilo la utoaji tuzo za EJAT 2013 mgeni rasmi anatarajiwa kuwa rais wa mahakama ya Afrika Mashariki, Jaji Harold Nsekela.