Na Khamis Amani
JAJI Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amewataka majaji, mahakimu na makadhi, kujirekebisha katika utendaji wao wa kazi ili jamii iweze kuwaamini.
Alisema utendaji dhaifu uliopo kwa baadhi yao, unashusha imani ya mahakama kwa wananchi.
Aliyasema hayo katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi,katika mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya majaji, mahakimu na makadhi Zanzibar (ZAJOA).
Alisema lawama nyingi za jamii zimekuwa zikitupiwa mahakama kwa kubatilisha haki na suala hilo lote linatokana na udhaifu wa utendaji kwa baadhi yao .
Aidha alisema suala hilo lilidhihiri wazi na kushuhudiwa na wao wote katika kilele cha siku ya sheria Zanzibar, ambapo hutuba nyingi zilizotolewa ziliilenga mahakama.
"Ni vyema tukajirekebisha vyenginevyo kila siku tutakuwa wahanga,”alitanabahisha.
Kuhusiana na Jumuiya hiyo,aliwataka wanachama kushikamana na kushirikiana katika kuiendeleza jumuiya hiyo, ambayo tayari imeshapiga hatua kubwa ndani na nje ya nchi.
Alitanabahisha fitna na majungu ni mambo ya kutupiliwa mbali kwani ni kikwazo cha maendeleo na hayawezi kusaidia chochote katika kuiimarisha taasisi hiyo.
"Najua bado kikundi cha mahakimu wachache wa mahakama ya mwanzo kipo na kinaendeleza fitna na majungu kwa kushirikiana na baadhi ya majaji na mahakimu wa ngazi nyengine ili kuua taasisi hii pamoja na kuiletea aibu mahakama," alitahadharisha.
"Napenda niwaeleze kuwa mimi nawajua na kama Mkuu wa muhimili huu wa mahakama nitakuwa tayari kupambana nao kwa hali zote, mimi sitakubali kuona taasisi hii ya ZAJOA inakuwa inashinikizwa na hawa watu wachache," alionya.
Aliwaomba majaji, mahakimu na makadhi wote wawe macho na wenzao hao ambao hawaitakii mema ZAJOA, na wana dhamira mbaya ya kuwavuruga huku akiwaasa mahakimu wapya walioapishwa hivi karibuni kutojiingiza katika mtego huo.
Aliwataka wanajumiya hiyo kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati yao na Jumuiya nyengine za Afrika Mashariki, katika kufanya kazi pamoja na kuendeleza ushirikiano zaidi.