Na Kauthar Abdalla
ASKARI Polisi E5607 Koplo Mohammed Mjombo (44), ameuawa na mwengine kujeruhiwa baada ya kupigwa risasi na majambazi katika tukio la uporaji lililotokea hoteli ya Pongwe Bay Resort iliyopo Pongwe wilaya ya kati Unguja.
Hoteli hiyo inamilikiwa na raia wa Italia alietambuliwa kwa jina la Giovanni Rundo.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 2:30 wakati majambazi hayo yaliyokuwa na silaha yalipovamia hoteli hiyo kwa lengo la kupora.
Aliejeruhiwa ametambuliwa kwa jina la PC Ibrahim Juma (35).
Kwa mujibu wa mashuhuda, kabla ya majambazi hayo kumuua askari huyo, waliwaweka chini ya ulinzi walinzi wa kimasai wanaolinda hoteli hiyo.
Walisema baada ya kuwaweka chini ya ulinzi walikwenda alipokuwepo mmoja ya askari hao na kumtaka asalimishe silaha yake, hata hivyo alikataa ndipo walipomdhibiti na kumjeruhi kwa kumpiga risasi ya bega na kuchukua silaha yake.
Walisema kutoka na mlio wa risasi askari mwengine aliekuwa sehemu nyengine ya lindo ndani ya hoteli hiyo, alikoki silaha yake lakini wakati akijiandaa kuvyatua risasi majambazi hayo ambayo hayajajulikana idadi yao, yalimuwahi na kumfyatulia risasi mbili zilizompata sehemu ya chini ya tumbo na paja.
Marehemu alichukuliwa na kukimbizwa hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu ambapo alifariki majira ya saa 9:00 usiku wakati akipatiwa matibabu.
Hata hivyo, baada ya kutekeleza unyama huo majambazi hayo yalikimbia kusikojuliana yakiwa na moja ya silaha walizompora askari wa kwanza.
Marehemu amezikwa jana kijijini kwao Bambi wilaya ya Kati na majeruhi anaendelea na matibabu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Augostino Ollomi, amethibitisha kutokea mauaji hayo na kusema watu watatu wanashikiliwa kwa mahojiano.
Aidha alisema hakuna mgeni yoyote aliejeruhiwa au kuibiwa katika tukio hilo .