NAHODHA wa timu ya Mkungu malofa Mussa Ali Mbarouk, akipokea kikombe cha ushindi wa michuano ya mwakilishi wa Jimbo la Chakechake, baada ya kuilaza timu ya Jagwakwa magoli 2-1, kutoka kwa Mohamed Juma Khatibu, kwa niaba ya mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe: Omar Ali Shehe, fainali ya michuano hiyo ilifanyika uwanja wa Polisi Madungu mjini Chakechake (picha na Haji Nassor, Pemba)
Na Haji Nassor, PEMBA
HATIMAE timu ya soka ya Mkugu malofa ‘Yosso’ imenyakua kombe la Mwakilishi Jimbo la Chakechake, baada ya kuiangusha timu ya Jagwa kwa magoli 2-1, kwenye mchezo wa fainali ya kusisimua uliochezwa uwanja wa Polisi Madungu.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, washindi walitangulia mbele kwa magoli mawili, ingawa baadae wapinzani walipata penalty na kujipatia goli la kufutia machozi, kwenye mchezo huo uliohudhuriwa na watazamaji wengi kiasi.
Mgeni rasmi katika kipute hicho Nd: Mohamed Juma Khatibu kwa niaba ya mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe: Omar Ali Shehe, alisema michezo hujenga urafiki, udugu na kuwa chanzo za ajira kwa vijana.
Alisema wengi wanadhani suala la michezo huishia uwanjani pekee, bali endapo vijana watajitolea na kuamua kucheza kwa kutafuta maisha, hilo linaweza kuwasaidia na kufikia malengo yao pasi na ajira kupitia serikali kuu.
Khatibu alisema, nia ya mwakilishi wa Jimbo la kuendeleza mashindano kwa miaka saba mfulululizo sasa, inafaa kungwa mkono na kila mmoja, ili ndoto za vijana wa Jimbo hilo la kuibua vipaji liweze kufikiwa.
‘’Naamini mfulululizo wa michuano hii kwa misimu saba sasa, basi wapo baadhi ya vijana wameshajiweka sawa kimichezo, lililobakia ni kuhakikisha tunamsaidia mwakilishi wetu afikie lengo alililolikusudia la kifichua vipaji’’,alisema.
Mshindi katika michuano hiyo pamoja na kombe, alikadhiwa shilingi laki 400,000 (laki nne), jezi seti moja na mipira, huku mshindi wa pili akiondoka na jezi seti moja, mipira na shilingi laki 300,000 (laki tatu), ambapo mshindi wa tatu timu ya Chake chake star, ilipata shilingi laki 2 na vifaa kama hivyo.
Michuano hiyo ya kuwania kombe la mwakilishi Jimbo ka Chakechake, ilioanza Januari 1 mwaka huu, ilizishirikisha timu 39, zikicheza kwa njia ya mtowano, ambapo baada ya kubakia timu nane zilicheza mtindo wa ligi na bingwa mtetezi ilikua ni timu hiyo ya Mkungu malofa.