Na Khamisuu Abdalla
KUWEPO idadi kubwa ya wazazi wanaozalia wodini katika hospitali kuu ya Mnazimmoja, linatokana na ongezeko la wajawazito katika hospitali hiyo.
Muuguzi dhamana wa wodi ya wazazi wa hospitali hiyo, Tatu Fundi Salum, alisema kuanzia mwezi Januari hospitali hiyo inazalisha kati ya wajawazito 70 hadi 89 kwa siku.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Mnazimmoja,muuguzi huyo alisema upungufu wa vitanda katika chumba maalum cha kuzalia ndio chanzo, kilichosababisha wajawazito kujifungulia wodini.
Aidha alisema kutokana na ongezeko la wazazi, kitanda kimoja kinatumiwa na wajawazito hadi watatu kwa wakati mmoja huku wodi nzima ikiwa na vitanda 47 pekee.
"Chumba cha kuzalisha (‘leba’) kina vitanda vitatu tu na kama unavyoona kwa siku tunazalisha watu wengi, leba kunajaa na kama mzazi yuko tayari kujifungua, tunalazimika kumzalisha palepale wodini,” alisema.
Alisema kufurika wajawazito katika hospitali hiyo kunatokana na wazazi kupuuza utaratibu uliowekwa wa kuzitumia hospitali nyengine kwa ajili ya kujifungua,ikiwemo hospitali za Muembeladu na Mpendae.
"Wodi ya wazazi sasa kama tumo sokoni wajawazito wengi sana na vitanda vyetu ni 47 tu havitoshelezi kwa wajawazito wote, sasa hutulazimu kuwaweka wajawazito hadi watatu katika kitanda kimoja,” alisema.
Alisema mzazi anapojifungua salama huwekwa kwa saa 6 kumchunguza zaidi huku wajawazito wanaozaa kwa upasuaji huwaweka kwa siku tatu.
Alisema kwa kawaida mzazi anapojifungua hutakiwa kubakia hospitali kwa saa 24 na wanaofanyiwa upasuaji hutakiwa kukaa siku tano.
Hata hivyo, alisema kiutararibu wazazi wanapojifungua mtoto wa pili hawatakiwi kwenda hospitalini hapo ikiwa watakua hahana matatizo, lakini wazazi wanakuwa wakaidi na hata ukiwarejesha waende hospitali nyengine huwa hawakubali.
Alisema kutokana na tatizo hilo, walipeleka maombi hopsitali ya KMKM Kibweni kupatiwa nafasi kwa ajili ya wajawazito na kukubaliwa lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa vifaa vya kuzalisha.
Hivyo aliiomba serikali kuwatafutia sehemu mbadala ya kuwajenga wodi ya wazazi kwa sababu hospitali ya Mnazimmoja haitoshelezi.
Pia aliwaomba wazazi waliowahi kujifungua katika hospitali hiyo, wazitumie hospitali nyengine za serikali ili kupunguza msongamano.
Wazazi 9 walipoteza maisha kwa kipindi cha Januari hadi Machi kutokana na kifafa cha mimba na kupoteza damu nyingi.