Na Rose Chapewa, MBEYA
POLISI Mkoani Mbeya, wamefyatua risasi kuwatawanya wananchi wenye hasira, waliokuwa wakijaribu kuwachoma moto wanawake wawili, waliowatuhumu kuwa wezi.
Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya,Ahmed Msangi alisema tukio hilo limetokea juzi saa 17.50. jioni eneo la la Mwanjelwa kata ya Manga, baada ya wanawake hao kuzingirwa na wananchi wakiwa kwenye duka la mfanyabiashara mmoja.
Aliwataja wanawake hao walionusurika kuuawa kuwa ni Rukia Rashind (24) Jamila Abdalah
(38),wakazi wa Tunduma wilaya ya Momba na kwamba wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
Alisema watuhumiwa hao waliingia katika duka la mfanyabiashara aitwaye Janeth Sivanus (28) wakiwa wamevalia nguo zinazoficha nyuosa zao na kuiba vitambaa vya vyenye thamani ya shilingi 2,400,000.
Alisema kabla ya kufanya wizi huo, wanawake hao waliuliza vitambaa hivyo na kisha mtuhumiwa mmoja alikwendelea kumsemesha muuzaji wa duka ambaye alikuwa akiendelea kuhudumia wateja wengine huku mtuhumiwa wa pili akiiba.
Alisema baada ya kuiba vitambaa hivyo na kuondoka pasipo mwenye duka kujua, majirani walimjulisha mwenye duka juu ya tukio hilo na ndipo jitihada zilianza za kuwafuatilia watuhumiwa hao na kufanikiwa kuwakamata karibu na nyumba ya kulala wageni ya Mfikemo iliyopo mtaa Jua Kali wakiwa na vitambaa hivyo.
Alisema baada ya kukamatwa lilijitokeza kundi la wananchi likiwa na silaha lililotaka kuwashambulia huku wakiwa na adumu ya petrol, lakini wakati wakijiandaa kutekeleza unyama huo polisi walifika na kufyatua risasi hewani kuwatawanya na kuwaokoa wanawake hao.
Kamanda Msangi alitoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani sio tabia nzuri na ni kinyume cha sheria.