Na Kadama Malunde,SHINYANGA
MAHAKAMA ya hakimu mkazi wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, imewahukumu Mathias Kalonga (40) na James Moshi (35) wakazi wa Shatimba wilaya ya Shinyanga vijijini, kifungo cha miaka 242 jela baada ya kupatikana na kosa la ubakaji kwa kundi,wizi wa kutumia silaha na kujeruhi.
Mwendesha mashtaka,wakili wa serikali Salome Mbuguni aliiambia mahakama hiyo jana kuwa mnamo tarehe 18 mwezi Oktoba,2012 washtakiwa wakiwa na wenzao walivamia nyumbani kwa mlalamikaji Lesha Jidomela,wakiwa na bunduki na mapanga kisha kumjeruhi kisha kupora simu tatu kinyume cha sheria hilo ikiwa ni kosa la kwanza na la pili.
Alidai katika kosa la tatu na nne washtakiwa hao wote kwa pamoja walivamia nyumbani kwa Sayi Jidomela(ndugu yake Lesha Jidomela) kisha kupora shilingi 57,000 na simu moja na mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa na panga kumjeruhi kwa kutumia panga hilo.
Aidha alidai katika kosa la tano na sita washtakiwa kwa pamoja walimbaka mke wa Lesha Jidomela kwa pamoja, lakini pia wakambaka mke wa Sayi Jidomela.
Mahakama ilisema upande wa mashtaka umethibitisha makosa dhidi ya washtakiwa pasipo na mashaka.
Akitoa hukumu,hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Thomson Mtani, alisema kutokana na kosa la wizi wa kutumia silaha kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela, hivyo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 60 kwa sababu kila mmoja alitenda kosa hilo katika nyumba mbili.
Alisema katika kosa la ubakaji kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na kwa kuwa wote kwa pamoja walibaka wanawake wawili kwa zamu kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 60.
Hakimu huyo alisema mshtakiwa wa kwanza Mathias Kalonga atatumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kujeruhi kwa panga na kutakiwa kulipa fidia ya shilingi 200,000 kwa waliojeruhiwa.
Kufuatia hukumu hiyo washtakiwa watatumikia kifungo cha miaka 242 jela,ambapo mshtakiwa wa kwanza Mathias Kalonga (40) atatumikia miaka 122 jela na mshtakiwa wa pili James Moshi (35) atatumikia miaka 120 jela na wote kwa pamoja kuchapwa viboko 12 kila mmoja.
Haki ya kukata rufaa imetolewa kwa upande usioridhika.