Na Joseph Ngilisho,ARUSHA
NAIBU wa Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba, amesema kukua kwa utandawazi kumeifanya dunia kuwa kijiji,hivyo kuna kila sababu ya kuimarisha majeshi ya ulinzi ya ndani kwa kushirikiana na majeshi ya nchi za nje kwa kuyaongezea ujuzi zaidi.
Kauli hiyo ameitoa jana katika mahafali ya kwanza ya kuhitimu kozi ya mafunzo mkakati kwa maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)kutoka chuo cha mafunzo ya kijeshi Monduli, baada ya kumaliza kozi ya mwaka mmoja katika chuo cha uhasibu Njiro,ambapo jumla ya maofisa 52 kutoka nchi 10 za Afrika walihitimu shahada ya uzamili na stashahada.
Alisema kwa sasa nchi nyingi za Afrika hazihitaji kupigana kwa ajili ya kupata uhuru ila zinahitaji ulinzi ili kupiga hatua katika masuala ya kiuchumi wakati nchi hizo zikiwa salama.
Hivyo alitoa rai kwa mafunzo hayo kuendelezwa zaidi katika program mbalimbali zitakazosaidia wahitimu kufanya vizuri zaidi katika kuimarisha utendaji wa kazi zao.
Alisisitiza lazima majeshi ya kiafrika yajiendeshe kisasa zaidi kwa kutumia elimu na ujuzi kutoka vyuo mbalimbali vya ndani na nje ili kwendana na hali ya utandawazi na teknolojia.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Prof.Johannes Monyo, alisema ushirikiano wa chuo na chuo cha kijeshi Monduli ulikuja kwa kutiliana saini mapema mwaka jana kutoa taaluma hiyo baada ya mitaala yake kupitishwa na taasisi ya elimu ya juu.
Alisema mafunzo hayo yatawasaidia wanajeshi hao na raia kuongeza ujuzi katika shughuli zao na kwamba chuo hicho kinatarajia kuanzisha programu nyingine ya mafunzo inayotarajiwa kuanza mapema mwakani,baada ya mtaala wake kukamilisha na kupitishwa.
Alisema makubalinao ya kuanzisha mafunzo hayo yanawezesha chuo hicho kupeana mafunzo juu ya kuboresha masuala mbalimbali ya kitaaluma ikiwemo sekta ya fedha,utawala na diplomasia.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaida pia kuwapa ujuzi wa kimkakati katika masuala ya kiuongozi,kutatua migogoro, usimamizi wa miradi, diplomasia,mawasiliano na sekta za kiraia na matumizi ya teknolojia.
Alisema chuo hicho kilianza kutoa kozi ya kwanza kwa maofisa wa jeshi zaidi ya 52 pamoja na wakufunzi kutoka TMA wanaotoka nchi mbalimbali zikiwemo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).