Na Mwandishi wetu
IDADI kubwa ya Watanzania ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 na vijana, utafiti wa mama na mtoto wa mwaka 2010 umebainisha.
Utafiti huo unaonesha asilimia 44 ya watu wote ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, huku kiwango cha uzazi kikiwa ni wastani wa watoto 5.4 kwa kila mama mwenye umri wa kuzaa ambao ni miaka 15-49.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa, alimueleza hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete Ikulu wakati akimkabidhi vitabu na majedwali yenye matokeo na machapisho ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Kulingana na takwimu, idadi ya watu Tanzania imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka watu milioni 12.3 mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012.
Aidha mkoa wa Dar es Salaam una asilimia kubwa ya vijana wenye umri wa miaka 15-35 wakati mkoa wa Singida ukiwa na asilimia ndogo zaidi.
Kulingana na takwimu, zaidi ya nusu ambayo ni asilimia 52.2 ya watu wote nchini, wako katika umri wa kufanya kazi ambapo mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya watu wenye umri huo na mkoa wa Simiyu uko chini zaidi kwa kuwa na asilimia 45.5 ya watu hao.
Katika takwimu hizo, zaidi ya nusu ya watu katika mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.
Alisema takwimu zinaonesha rasilimali watu kwa ajili ya kuzalisha na kuongeza uchumi na kupunguza umaskini sio tatizo na kinachotakiwa ni watu wote kutumia fursa zilizopo nchini kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuinua uchumi.
Kulingana na takwimu, asilimia 5.6 ya watu nchini ni wazee na takwimu hizo zinaonesha wazee kwa asilimia kubwa wako katika mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo asilimia ndogo zaidi wapo katika mikoa ya Dar es Salaam na mjini Magharibi.
Kwa mujibu wa sera ya wazee Tanzania, mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 au zaidi.
Alisema takwimu pia zinaonesha asilimia ya watu wanaoishi mijini imeongezeka zaidi ya mara tano ambapo ni asilimia 6.4 mwaka 1967 na kufikia asilimia 29.6 kwa mwaka 2012.
Jiji la Dar es Salaam lina asilimia 10 ya watu wote Tanzania Bara wakati mjini magharibi ina asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar .
Sensa pia imeonesha kuwa wanawake ni wengi zaidi, kwa asilimia 51 ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 49 kama ilivyo katika nchi nyingi barani Afrika.
Alisema mkoa wa Manyara unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanaume ambapo mkoa wa Njombe una idadi ndogo zaidi ya wanaume.