Na Mwandishi wetu
MGOMBEA wa CUF katika uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze,Fabian Skauki,amemuwekea pingamizi mgombea wa Chadema,Mathayo Mang’unda Torogey akisema amepoteza sifa ya kuwa mgombea.
Katika pingamizi yake kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mgombea huyo alisema Torongey amejaza taarifa za uongo kwenye fomu yake kwamba kazi anayoifanya ni biashara wakati sio kweli kwa sababu hajaweka vielelezo.
Aidha alisema mgombea huyo alisema anajua kusoma na kuandika kiswahili na kiingereza, taarifa ambazo ni za uongo na kwamba mgombea huyo hajui kusoma wala kuandika kiswahili seuze kiingereza, na kwamba amedanganya.
Hoja ya tatu alisema mgombea wa Chadema amedanganya kwa kughushi saini za wadhamini, ambao amewaorodhesha kwenye fomu ya kuomba kuthibitishwa kuwa mgombea.
Alisema katika fomu hizo wadhamini wote saini zao zimefojiwa na hazifanani na zile zilizokuwepo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba saini zote hizi zimesainiwa na mtu mmoja ambaye sio muhusika.
Hoja ya nne alisema mgombea huyo ameshindwa kutimiza mahitaji ya kisheria ya kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake amedhaminiwa na wadhamini 28 ambao kati yao wadhamini 7 sio wapiga kura halali wa jimbo la Chalinzi na kwamba taarifa zao na namba zilizojazwa hazifanani, hivyo anabakiwa na wadhamini halali 21 ambao kisheria hawatoshi kutimiza matakwa ya kisheria.
Ameiomba Tume ya Uchaguzi kutengua uteuzi wa mgombea huyo kwa kuwa anakosa sifa za kuendelea kuwa mgombea.