Na Salum Vuai, Maelezo.
BARAZA la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), jana limeadhimisha ‘Siku ya Kiswahili Zanzibar ’, huku serikali ikishauriwa kulisaidia kwa kuliwezesha kirasilimali ili litekeleze jukumu lake la kuhakikisha lugha hiyo inakua, kusambaa na kutumika kwa usahihi.
Akizungumza katika hafla fupi ya maadhimisho ya siku hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Kamisheni ya Michezo na Utamaduni Mwanakwerekwe, Naibu Mwenyekiti wa baraza hilo Mmanga Mjengo Mjawiri, alitaja changamoto mbili kuu zinazoikabili lugha hiyo.
Changamoto ya kwanza alisema, ni uhaba wa wataalamu wa lugha hiyo katika aina mbalimbali za tanzu zake, ikiwemo fasihi, sarufi, uandishi na nyengine, ambapo alieleza kuwa kunahitajika watu weledi na waliobobea katika kuzichanganua fani hizo.
Akifafanua, Mjawiri alisema, kuna watu wengi wanaojua kuzungumza Kiswahili, lakini hawana utaalamu wa tanzu zake, ambao wamekuwa wakisema lugha hiyo haina utaalamu, na kutaka watu kama hao waelimishwe.
Aliitaja changamoto nyengine, kuwa ni ukosefu wa rasilimali fedha, akisema suala hilo linahitaji kushugulikiwa kwa namna ya pekee kwani katika jitihada za kukistawisha Kiswahili na kukiongezea hadhi na miongoni mwa mataifa mbalimbali.
Naibu huyo Mwenyekiti wa BAKIZA alitoa mfano wa nchi nyengine, akisema huwa zinaziwezesha vyema Idara zinazoundwa kushughulikia maendeleo ya lugha zao kwa kujua umuhimu wao.
“Kama kweli tunakusudia kukikuza Kiswahili na kukisambaza hata nje ya nchi, ni lazima mamlaka husika zioneshe dhamira ya dhati kuliwezesha baraza kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” alisisitiza.
“Kudhani kama Kiswahili kitajiendeleza chenyewe bila msaada wa mamlaka, jamii na serikali si dhana sahihi, kunahitajika nguvu kubwa ya pamoja katika kuifanya kazi hii,” alifahamisha.
Aliitaka BAKIZA kuongeza kasi zaidi kwa kutanua wigo wa kukiendeleza, na kwamba hata maadhimisho ya siku ya Kiswahili yanapaswa kufanyika kwa ukubwa zaidi badala ya hafla ndogo za kuwazawadia waandishi wa insha na mambo kama hayo.
Alisema katika wakati huu ambapo Kiswahili kinazungumzwa na watu wengi sana wapatao milioni 150 kote duniani, huku wenye lugha yao wakikipa uzito hafifu, kunawafanya watu wengine kuja na misamiati yao mipya, na kujifanya wao ndio wataalamu.
Kwa upande mwengine, Mjawiri alisema watu wanaiona lugha kama ni fani isiyokuwa na thamani kwa maana ya kifedha kama ilivyo kwa vitu vyengine vinavyoweza kuuzwa na kununuliwa, lakini akaeleza kwamba kama serikali itakuwa na mikakati mizuri, Kiswahili kinaweza kusaidia kukuza uchumi wa jamii na taifa wa jumla.
Alitoa wito kwa wananchi hasa wanafunzi, kujenga utamaduni wa kusoma vitabu vya Kiswahili na lugha nyengine, wakianzia vya waandishi wa Zanzibar, Tanzania, Afrika Mashariki, na hatimaye Afrika na duniani kwa jumla ili kujifunza misamiati mipya.
Aidha aliwashauri wananchi wenye uwezo kujikita katika uandishi wa vitabu vya fani mbalimbali ikiwemo tamthilia ambayo alisema bado haijapewa uzito unaostahili kulinganisha na fani nyengine kama ushairi na riwaya.
Mapema, Katibu Mtendaji wa BAKIZA Khadija Bakari Juma, alisema ilikuwa nia ya baraza hilo kuadhimisha siku ya Kiswahili kwa kufanya mambo makubwa, lakini kutokana na matatizo yaliyo nje ya baraza hilo, wamelazimika kuandaa hafla hiyo ndogo.
Aliwaomba wananchi kukinunua kitabu kipya kilichoandikwa na watalamu wa BAKIZA kwa kushirikiana na wadau wake, kiitwacho ‘Kiswahili kwa wageni’, ambacho pia kilizinduliwa rasmi katika hafla hiyo.
Kabla ya hapo, BAKIZA ilichapisha vitabu mbalimbali, ambavyo ni Utamaduni wa Mzanzibari (2008), Kamusi la Kiswahili Fasaha (2010), Makala za Semina ya Kumuenzi Bwana MSA (2011), Kamusi la Lahaja ya Kimakunduchi (2012), Kamusi la Lahaja la Kipemba (2012), Kamusi la Lahaja la Kitumbatu (2012) na Jarida la BAKIZA (2013).
Maadhimisho hayo ya Siku ya Kiswahili Zanzibar, yaliambatana na utoaji zawadi kwa washindi wa uandishi wa insha, ambapo mshindi wa kwanza alikuwa Azya Daudi Mkasha wa skuli ya Biashara Zanzibar, wa pili ni Omar Mrisho Abdalla wa skuli ya sekondari Uroa na Mariam Makame Nyange kutoka skuli ya Biashara Zanzibar aliyeshika nafasi ya tatu.
Maadhimisho ya siku ya Kiswahili Zanzibar hufanyika ifikapo tarehe 13 Machi ya kila mwaka.