Na Madina Issa
BARAZA la Wazee la Chama cha Mapinduzi Zanzibar, limeelezea kusikitishwa na kitendo cha Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, kusaini waraka unaopendekeza muundo wa muungano wa serikali tatu katika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji wa baraza hilo Zanzibar, Haji Machano Haji, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kuu za CCM, Kiswandui mjini Unguja.
Alisema wazee hao walishitushwa na kufadhaishwa na msimamo wa Spika huyo ambapo hapo awali alidai kuwa hakuutambua waraka huo licha ya kuwa na saini yake na hatimae kwenda kuuwasilisha kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Aidha alisema kwa kuzingatia uzoefu wa medani za siasa na hasa za Zanzibar, hali hiyo imewashitua na kuiona sio ya kawaida tangu kuasisiwa kwa Baraza la Wawakilishi mwaka 1979.
Alisema tokea muda huo hawajawahi kumsikia kiongozi wa taasisi hiyo muhimu (Spika) kuwa na kauli mbili katika jambo zito ambalo linagusa maslahi ya nchi.
"Kwa mantiki hii sisi wazee tunajiuliza hivi inawezekana kweli baraza la Wawakilishi kufikia maamuzi ya jambo zito linalogusa maslahi ya nchi bila ya kuitishwa kikao rasmi hatimae kufikia maelewano ya pamoja au kwa kupigiwa kura," alisema.
Alisema kwa uzoefu wa muda mrefu wanafahamu vikao vya Baraza la Wawakilishi hufanywa wazi na wajumbe hupata nafasi ya kujadiliana na baadae kutoa uamuzi.
Aaliwasihi viongozi wa vyama vya siasa kutambua kwamba wametumwa na wananchi kuwakilisha na kuongoza kwa haki na kwa uadilifu kwa kuzingatia katiba ya nchi na sio kuendesha nchi kwa ungovi na chuki.
Hata hivyo, wazee hao walisema baraza lao linapendekeza kuendelezwa muungano wa serikali mbili.