Na Mwandishi wetu
POLISI Mkoa wa Kusini Pemba, linamshikilia Ali Faki Ali (22) mkazi wa Wawi Umangani,kwa kujifanya Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwapatia mafunzo ya kijeshi vijana na kisha kuwatapeli shilingi milioni 4.5.
Kamanda mpya wa polisi mkoa huo, Yussuf Juma Ali, alisema, mtuhumiwa alikamatwa kijiji cha Umangani Wawi wilaya ya Chake Chake.
Alisema mtuhumiwa mwenyeji wa Bumbwini wilaya ya Kaskaazini B, Unguja, alikusanya vijana hao kutoka Unguja na Pemba akiahidi kuwa atawapatia ajira za jeshi na kuwataka kila mmoja kulipa shilingi 800,000.
Alisema baada mtuhumiwa huyo aliwakusanya vijana hao nyumbani kwake na kuwapa mafunzo ya awali ya kijeshi akiwambia ni maandalizi kabla ya kujiunga na mafunzo kamili ambayo yangefanyika Kigoma.
Alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha alisema watu watatu wanaotuhumiwa kuwa majambazi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuvamia nyumba ya raia mmoja wakiwa na silaha aina ya SMG na bastola.
Alisema katika tukio hilo majambazi hayo yalimjeruhi mtoto wa mwenye nyumba hiyo sehemu ya usoni na kupora simu na fedha taslimu shilingi 100,000.
Wakati huo huo, Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, wanawashikiliwa watu 15 wanahusishwa na kundi la ubaya ubaya kwa kuhusika na tukio la kufunga barabara katika eneo la Mwanakwerekwe wiki iliyopita.
Alisema katika tukio hilo, vijana kutoka kundi hilo, walifunga barabara hiyo baada ya askari wa vikosi vya SMZ kwa kushirikiana na maafisa kutoka Idara ya Mazingira kuwakamata vijana wakichota mchanga kwa kutumia gari la ng’ombe.
Alisema ili kulipiza kisasi, vijana wa kundi hilo walivamia eneo hilo na kufunga barabara kurusha mawe na marungu kwa gari zilizotumia barabara hiyo.
Katika tukio hilo gari mbili za serikali, zinazomilikiwa na Wizara ya Fedha na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) pamoja na gari moja linalomilikiwa na mtu binafsi ziliharibiwa kwa kuvunjwa vioo vya mbele na nyuma.