Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM
RAIS Mstaafu na mlezi wa Taasisi ya Walimu wanaofundisha Qur-an Tanzania (JUWAQUTA), Ali Hassan Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la Mashekh na Wanazuoni, litakalojadili mfumo wa kiuchumi wa kiislam,fursa pamoja na changamoto.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa JUWAQUTA taifa,Shekh Alhad Salum, alisema kongamano hilo litafanyika Machi 18 hadi 19 katika ukumbi wa Karimjee.
Alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili la uchumi wa kiislam ambao umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo riba katika mikopo,hivyo kusababisha baadhi ya waislamu kutonufaika na mikopo itolewayo na taasisi za fedha.
“Tuna changamoto kubwa katika benki zetu kutokana na kuwa na riba jambo ambalo linaleta shida kwa jamii ya kiislamu kutoweza kunufaika nayo,”alisema.
Alisema kongamano hilo litatoa fursa kwa jamii ya kiislamu na wasiokuwa waislamu kufahamu mfumo wa kiuchumi wa kiislamu kwa mujibu wa Qur-an na sunna na kaungalia ni namna gani mfumo huo unaweza kutumika sambamba na mfumo uliopo sasa kwa manufaa ya wote.
Kongamoano hilo limeandaliwa na Taasisi ya Walimu wanaofundisha Qur-an Tanzania (JUWAQUTA) na litajumuisha Mashekh na Wanazuoni maarufu nchini na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao.