Na Kija Elias, MOSHI
BENKI ya Damu imezionya hospitali zenye tabia ya kuwauzia damu wagonjwa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Meneja wa kituo cha damu salama kanda ya kaskazini, Dk. Wilhellmuss Mauka, wakati wa zoezi la uchangiaji damu kwa hiari kutoka kwa vijana zaidi ya 50 wa kanisa la Waadventista Wasabato Majengo manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema kuna urasimu unaofanywa na baadhi ya watendaji wa hospitali kuchukua fedha kutoka kwa wagonjwa ambao wamepungukiwa damu kitendo ambacho ni kinyume chaa maadili ya uuguzi.
“Ni kweli kuna baaadhi ya hospitali zimekuwa zikiwauzia wagonjwa damu, kitendo hiki ni kibaya, damu siyo kitu ambacho anaweza akapewa kila mgonjwa mwenye upungufu wa damu, na upatikanaji wake sio kwa fedha,” alisema.
Alisema katika hospitali kuna maalumu wanaokabidhiwa chupa za damu lakini cha kushangaza wamekuwa wakiuza kwa wagonjwa, tena kwa fedha nyingi.
Alisema serikali imekuwa ikitumia shilingi 225,000 hadi 600,000 kwa ajili chupa moja ya damu ikiwani ni pamoja na kuzikusanya na kuzifanyia tafiti, lakini cha kusikitisha watu hao wasio waaminifu huuza kwa shilingi 20,000.
Aliwashukuru vijana wa Sabato walioonesha nia ya kujitolea damu na kusema mchango wao utasaidia kupunguza upungufu unaoikabili benki ya damu.
Kwa upande wake mzee wa kanisa la Adventista Wasabato Majengo, Raphael Mseja, alisema bado jamii haijawa na mwamko wa kujitolea katika kuchangia damu kwa hiari na kutoa rai kwa Watanzania kuona umuhimu wa kujitolea ili kunusuru maisha ya mama na watoto.